Makachero wamnasa polisi feki Dagoretti Kusini
MAAFISA wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Riruta, Eneobunge la Dagoretti Kusini, Kaunti ya Nairobi wamemtupa korokoroni mwanaume wa umri wa miaka 26.
Ni baada ya kumkamata akiwa na kofia ya polisi, bastola nne bandia, shoka miongoni mwa vifaa vingine katika eneo la Dagoretti Corner.
Polisi walimfumania James Kariuki, Oktoba 4,2024 akiwa kwenye pikipiki na mweznake ambaye alifanikiwa kuchana mbuga baada ya umma kuwafahamisha.
Kulingana na Kamanda wa Polisi eneo la Kabete Bw Kivindu Kalonzo, wawili hao walikuwa kwenye pikipiki katika eneo la Dagoretti Corner wakielekea katika mtaa wa Kabiria unaotajwa kuwa na visa vingi vya uhalifu.
“Polisi walifanikiwa kumkamata mwanaume mmoja, mwenzake ambaye aliruka kwenye kwenye pikipiki na kutoweka anatafutwa na maafisa wa polisi. Wakati wa kumkamata alikuwa na bastola bandia zinazoaminika kutumika kufanya uhalifu,” alisema Bw Kivindu.
Bw Kivindu alisema polisi walipekua begi la mshukiwa na kumpata na silaha kinyume na sheria.
“Maafisa wetu wataendelea kufanya uchunguzi zaidi na kushika doria katika maeneo ambayo uhalifu unatekelezwa. Huyu kijana atatusaidia kujua anafanya kazi na nani?” alisema Bw Kivindu.
Tukio hilo lilihusisha maafisa wa upepelelezi huku mshukiwa akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Riruta.