Habari Mseto

Makarani walilia malipo ya kusajili watu Huduma Namba

July 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

MAKARANI waliofanya kazi ya kusajili Wakenya kwa ajili ya Huduma Namba mwezi uliopita wameshutumu serikali kwa kuchelewesha malipo yao.

Katika wilaya ya Rachuonyo, Kaunti ya Homa Bay, makarani zaidi ya 120 na wasimamizi wa usajili (RO) 20 walisema kuwa serikali haijawalipa jumla ya Sh2.3 milioni.

Kulingana na Bw Martin Njoga aliyekuwa karani wa shughuli hiyo iliyofanyika kati ya Aprili 2 na Mei 25, 2019, maafisa hao wa usajili wamepokea malipo ya siku 35 walizofanya kazi lakini bado serikali haijawalipa malipo ya siku 17.

Hali ni sawa na hiyo katika Kaunti ya Kakamega. Katika Kaunti ya Kisumu, makarani walioendesha shughuli hiyo walisema hawajapokea malipo ya siku zilizoongezwa na Rais Kenyatta kuwawezesha Wakenya kukamilisha usajili huo.

Katika Kaunti ya Kisii, makarani pia walilalama kuwa hawajalipwa hela za siku saba zilizoongezwa na Rais Kenyatta baada ya makataa.

“Tumelipwa mara tatu. Mara ya kwanza kila karani alilipwa Sh20,000. Mara ya pili tuliwapa Sh15,000 na awamu ya tatu walipewa Sh10,000. Bado hatujawalipa hela zilizosalia. Tunasubiri mawasiliano kutoka Nairobi,” akasema Naibu Kamishna wa Kisii ya Kati Bw Leonard Mgute.

Kulingana na barua inayodaiwa kuandikwa na wizara ya Masuala ya Ndani mnamo Mei 31, 2019, makamishna waliagizwa kuhakikisha kuwa makarani waliopoteza au kuharibu vifaa vya usajili wanalipa kabla ya kupewa malipo yao.

“Lengo la barua hii ni kuwaagiza kuwakata fedha makarani waliopoteza au kuharibu vifaa vya usajili,” akasema inasema barua hiyo ambayo haijapigwa muhuri wa serikali. Kulingana na barua hiyo, makarani waliopoteza au kuharibu vifaa vya kusajili watu kwa njia ya kielektroniki watatakiwa kulipa karibu Sh90,000.

Kwingineko, watawala katika kaunti ya Pokot Magharibi wameagizwa washughulike   kuwasajili watoto wote wachanga eneo hilo.

Kwenye uzinduzi wa shughuli ya siku 30 ya kutoa huduma kwa haraka (RRI), Naibu wa kamishina katika kaunti ndogo ya Pokot Magharibi, Bw Abdulahi Khalif, alisema ni lazima kila mtoto asajiliwe. Kauli ya Bw Khalif inatokana na agizo la Wizara ya Usalama wa ndani.

Wakati wa uzinduzi huo eneo la Makutano, Bw Khalif aliwataka machifu na manaibu wao wachukue hatua za haraka kuhakikisha jambo hilo linafanyika.

“Tuna idadi kubwa ya vyeti 56,000 ambavyo havijachukuliwa na ni jukumu letu sisi sote kuzishughukia kwa siku 30”, alisema Bw Khalif.

Naibu huyo wa kamishna alitoa onyo kali kwa machifu na manaibu wao wakiwemo wazee wa mitaa dhidi ya kujihusisha kwenye maovu ya kuchukua mlungula kutoka kwa wakazi kwenye zoezi hilo.

“Tumepokea malalamishi mengi kuhusu fedha ambazo zinachukuliwa na machifu na tunawasaka.Sitaki shoka liangukie wengine wetu na ni afadhali tuachane na tabia hilo ,”akasema Bw Khalif.

Bw Khalif aliwaonya machifu kuhsuu kuchukua hongo kutokana na maombi ya sensa.

Maafisa wa Huduma Centre waliwataka wakazi wafike hapo ili kupokea huduma kutoka kwa kituo hicho kipya ili kuweza kusajili miradi ya ujenzi wa nyumba ambapo idadi ya wakazi 15,000 kutoka kila kaunti wanalengwa.