Mama aliyekaribisha Gachagua kunywa chai kwa kibanda chake apewa Sh100,000
MAISHANI mwake, Bi Asha Chengo, muuzaji wa vyakula kwenye kibanda kidogo katika bustani ya Mama Ngina iliyoko Mombasa, hakuwahi kufikiria kungetokea siku ambapo angekaa na Naibu Rais, kunywa naye chai na kupiga gumzo.
Mwaliko wa chai alioutoa kwa Naibu wa Rais, Bw Rigathi Gachagua, Alhamisi ulimpa nafasi murwa ya kutangamana naye katika makazi rasmi ya Naibu Rais jijini humo.
Akiwa katika matembezi katika bustani ya Mama Ngina, Bw Gachagua alikuwa amemwona na kumsalimia Bi Chengo kutoka mbali.
Licha ya hayo, siku yake ilikuwa imechukua mkondo tofauti baada ya Bw Gachagua kumpa mwaliko, uliompa nafasi ambayo Mkenya yeyote angeifurahia.
“Ulipopita, nilijiambia, huyu lazima ni Naibu wa Rais. Niliomba mwenyezi Mungu anipe ujasiri wa kukueleza shida zangu nikiwa na matumaini kuwa ungenisaidia. Nilikukaribisha unywe chai, na nikaduwazwa kuwa ulinisikia,” akasema Bi Chengo wakati wa kupiga gumzo na Naibu wa Rais.
Kwa Bi Chengo ambaye hufanya kazi ya kuuza vyakula katika jiji hilo la kitalii, ilikuwa nafasi mwafaka ya kueleza matataizo yake, akiwa na imani kuwa Bw Gachagua angemsaidia.
“Mimi hupika chapati, ugali na vyakula vingine. Ni mzaliwa wa Kaunti ya Kilifi na huku Mombasa nimekuja kujitafutia riziki. Nimekuwa nikipitia matatizo na wanangu na siku ya kwanza ulipopita sikuwa na uwezo wa kukusimamisha kwa kuwa mvua ilikuwa ikinyesha,” akasema Bi Chengo.
Bi Chengo alimweleza Naibu wa Rais kuwa mmoja wa wanawe alikuwa hajajiunga na shule ya sekondari kwa sababu ya kukosa karo.
Mwanawe wa pili naye alikuwa amejiunga na shule kwa kuwa alibahatika kupata basari ila isingetosha kulipia karo yote.
Katika jibu lake, Bw Gachagua alitoa ufadhili wa kifedha na kumchochea kupanua biashara yake ili awasomeshe wanawe.
“Nitakupa Sh100,000. Nusu ya hela hizi uwapeleke watoto shuleni na nusu yake uwekeze katika biashara yako ili uweze kuwashughulikia wanao,” akasema Bw Gachagua.