Habari MsetoSiasa

Mama wa Taifa aongoza usajili wa Huduma Namba Ikulu

April 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

PSCU na CHARLES WASONGA

MAMA wa Taifa Bi Margaret Kenyatta Jumatatu aliongoza wafanyakazi wa Ikulu katika shughuli ya kusajiliwa katika mpango wa Huduma Namba.

Baadhi ya waliosajiliwa baada ya Mkewe Rais ni Msimamizi wa Ikulu Kinuthia Mbugua, Mkuu wa Wafanyakazi katika Afisi ya Mama wa Taifa Constance Gakonyo na Naibu wa Msimamizi wa Ikulu George Kariuki.

Wengine walikuwa Msaidizi wa Rais Kenyatta, Jomo Gecaga, na Mlinzi wa Rais Luteni Kanali Timothy Stelu Lekolool.

Hafla hiyo ilifanyika katika Ikulu ya Nairobi ikiongozwa na timu ya wasajili kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani na Ushirikishi wa Serikali ya Kitaifa chini ya Faith Onyango ambaye ni Afisa anayesimamia Mfumo Shirikishi wa Kitaifa wa Kujitambulisha jijini Nairobi, almaarufu NIIMS.

Rais Kenyatta alizindua shughuli hiyo ya usajili wa Huduma Namba Jumanne wiki iliyopita katika eneo la Masii katika Kaunti ya Machakos kwa kusajiliwa yeye mwenyewe na kuanzisha usambazaji wa vifaa vya usajili katika kaunti zote 47.

Mpango huu wa usajili una lengo la kuwatambua watu wote wanaoishi humu nchini wakiwemo wageni kupitia kwa kitambulisho kimoja cha kimsingi kwa kutumia data maalum hasa alama za vidole, picha ya uso, habari za kibinafsi na maumbile. Kupitia mpango huu, serikali inalenga kuimarisha mikakati yake ya kudhibiti usalama wa kitaifa.

Nambari hiyo mpya haitasitisha bali italeta uwiano na taratibu zingine za usajili wa kitaifa, kama vile, vitambulisho vya kitaifa, Bima ya Kitaifa ya Hospitali, Hazina ya Malipo ya Uzeeni, vyeti vya Kuzaliwa na Kifo au Namba ya Kitambulisho ya Kulipia Ushuru (PIN) kati ya nambari nyinginezo.

Pia Huduma Namba ina lengo la kurahisisha kasi na ubora wa utoaji huduma kwa Wakenya wote na itajumuisha pamoja namba zingine zote za usajili katika mfuko mmoja wa kidijitali. Namba hizo zingine zitachukua nafasi ya pili katika kumtambulisha mtu.

Akizungumza katika uzinduzi wa shughuli hiyo wiki iliyopita, Rais Kenyatta alisema mfumo huu wa usajili utaboresha na kuimarisha usajili wa wanaozaliwa na wanaofariki na usimamizi wa habari za mtu.

Aidha, akasema Rais Kenyatta, Huduma Namba pia utafanikisha vita dhidi ya ufisadi kando na kuharakisha utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.