Mama, watoto wake waliofukua mwili wa baba yao washtakiwa kortini
MAMA mwenye umri wa miaka 51 na watoto wake waliofukua mwili wa marehemu baba yao, walishtakiwa, Jumanne, Aprili 8, 2025 katika Mahakama ya Eldoret kwa kushiriki kitendo cha kuogofya bila kuwa na kibali.
Sally Tanui ambaye ni mke wa marehemu pamoja na watoto wake, William Cheruiyot, Abraham Kipyego, Faith Jepng’etich na Dickson Kipchirchir walishtakiwa kwa kufukua maiti bila kibali kinyume na kifungu cha 146 (1) cha Sheria ya Afya ya Umma.
Mahakama iliambiwa kuwa kati ya Aprili 5 na 6 katika kijiji cha Leseru kwenye Kaunti ndogo ya Turbo, wanne hao walisumbua maiti ya Noah Tanui aliyefariki akiwa na umri wa miaka 52 na kuzikwa 2010.
Upande wa mashtaka uliambia mahakama kuwa washtakiwa walifukua mabaki ya mwili huo kutoka kaburini bila kibali.
Wakiwa mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Eldoret, Kesse Cherono washtakiwa hao, akiwemo mama yao walikubali shtaka hilo mbali na Dickson Kipchirchir aliyekanusha shtaka husika.
Hakimu aliamuru washtakiwa wazuiliwe katika Gereza la Eldoret GK wakisubiri kusomewa maelezo ya mashtaka kwa wale waliokiri makosa na pia kutoa uamuzi wa kuachiliwa kwa dhamana kwa aliyekana shtaka hilo.
Bi Tanui pamoja na watoto wake baada ya kukiri kosa, walikiri kwamba walilazimishwa na ugumu wa maisha uliotokana na mzozo wa ardhi ambapo marehemu alizikwa.
Kwenye mahojiano na Taifa Dijitali, walilaumu polisi na viongozi kutoka eneo hilo kwa kuwatenga na kuacha mtu ambaye anataka kunyakua shamba lao kuendelea kuwanyanyasa licha ya kujua ukweli kuhusu ardhi hiyo.
“Hatua ya watoto wangu kufukua mwili wa baba yao ilitokana na mateso ambayo wanapitia baada ya baba yao ambaye aliwapenda zaid kufariki, hatua hii ililenga kuambia ulimwengu kuwa tunadhulumiwa,” akasema Bi Tanui.
Aliongeza kuwa watoto wake walitaka kutoka kwenye boma hilo na mwili wa marehemu kama mtu wa pekee ambaye aliwapenda sana katika ulimwnegu huu.
Kesi hiyo itatajwa mnamo Aprili 9.