Habari Mseto

Mamilionea wang'ang'ania dhahabu ya jangwani

April 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANDISHI WETU

MATAJIRI kutoka Nairobi wamefurika katika Jangwa la Chalbi, karibu na Ziwa Turkana kununua ardhi, baada ya kugunduliwa kwa kiasi kikubwa cha dhahabu na almasi chini ya ardhi.

Duru za kuaminika zimearifu Taifa Leo kuwa kuna wakubwa serikalini ambao walipata habari kuhusu uchunguzi uliofanywa na shirika la Duster Gold Find Inc, ambao ulionyesha kuwa eneo hilo lenye ukubwa wa kilomita 100,000 mraba lina kiasi kikubwa cha dhahabu na almasi hata kushinda inayopatikana Afrika Kusini.

Baada ya kupata habari za uchunguzi huo, maafisa hao wameanza kununua vipande vikubwa vikubwa vya ardhi eneo hilo wakishirikiana na rafiki zao.

Wenyeji waliambia mwanahabari wetu kuwa tangu mwezi jana wamekuwa wakiona helikopta zikitua eneo hilo karibu kila siku, na pia kuna masoroveya ambao wameanza kugawa vipande vya ardhi vya ekari kumi kumi.

Mmoja wa mabilionea wa Nairobi ambaye tayari amenunua ekari 100, alieleza Taifa Leo kuwa ekari moja inauzwa kwa Sh10 milioni.

“Ninatarajia kuuza ardhi hii baadaye mwaka huu kwa Sh100 milioni kwa kila ekari. Tuko wachache wale tuko na habari hizi na wakati serikali itakapotangaza kuhusu kiasi kikubwa cha dhahabu na almasi iliyoko Chalbi, matajiri kutoka ng’ambo watatua hapa kwa fujo. Wale tumenunua tunasubiri kupata faida ya ajabu,” akasema Dickson Mureithi.