• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Marafiki wamsaidia Jowie kuchanga Sh2m za dhamana

Marafiki wamsaidia Jowie kuchanga Sh2m za dhamana

Na Richard Munguti

MSHUKIWA mkuu katika mauaji ya mfanyabiashara aliyekuwa akihudumu Sudan Kusini Monicah Kimani, Joseph Irungu almaafuru Jowie, aliachiliwa Alhamisi kwa dhamana baada ya kukaa gerezani siku 500.

Jaji James Wakiaga alimwachilia Jowie kwa dhamana ya Sh2 milioni pesa tasilimu, ambazo alisaidiwa na marafiki kuchanga.

Jowie, sasa yuko huru sawa na mpenziwe Jacqueline Maribe wanayeshtakiwa pamoja kwa mauaji ya Monicah usiku wa Septemba 19, 2018 katika makazi yake, Lamuria Gardens eneo la Kilimani Nairobi.

Jowie alikuwa amenyimwa dhamana hapo awali kwa madai atawavuruga mashahidi na kuhepa.

Mahakama ilisema mashahidi waliohofiwa watavurugwa na Jowie tayari wametoa ushahidi na “hofu iliyokuwa haipo tena.”

Akinyimwa dhamanaa hapo awali, Jowie alidaiwa ni hatari kwa usalama wa mashahidi waliokuwa wameorodheshwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo inayowakabili yeye na mpenziwe Jacqueline Maribe.

Jacqueline, ambaye ni mwanahabari , alikuwa ameajiriwa na kituo kimoja cha Televisheni cha humu nchini.

Ilimbidi aache kazi kupambana na kesi ya mauaji inayomkabili pamoja na mpenziwe Jowie.

Akimwachilia kwa dhamana, Jaji Wakiaga anayesikiza kesi hiyo alimwamuru Jowie awe akipiga ripoti kila Alhamisi ya kila mwezi kwa Chifu wa eneo atakapokuwa akiishi.

Chifu huyo ameagizwa awe akiwasilisha ripoti kwa naibu wa msajili wa Mahakama kuu iwapo mshtakiwa ametii masharti ya kuachiliwa kwa dhamana.

Pia alimwagiza Jowie asijadili kesi hii katika mitandao ya kijamii ama katika chombo kingine chochote cha habari hadi isikizwe na kuamuliwa.

Mahakama ilisemaa kufikia sasa hakuna sababu maalum inayoweza kuzuia mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Mahakama ilisema tayari mashahidi 15 wamefika kortini na kutoa ushahidi dhidi yake.

Jowie aliamriwa awasilishe pasipoti yake mahakamani.

Pia aliamriwa asisafari nje ya nchi hii bila kupata idhini ya mahakama.

Mahakama iliamuru kwamba iwapo Jowie hatatekeleza masharti hayo basi dhamana aliyopewa itafutiliwa mbali na kuzuiliwa rumande.

Jowoe alitiwa nguvuni Septemba 26, 2018 kwa kushukiwa alimuua Monicah.

Monicah aliuawa kinyama kwa kukatwa koo na mwili wake kutupwa ndani ya beseni ya kuogea kando ya chumba chake cha kulala.

Hata hivyo, baadhi ya Wakenya wengi mitandaoni walihusisha kuachiliwa kwa Jowie na matamshi ya kinara wa ODM Raila Odinga ya ‘Jowi, Jowi, Jowi’ wakati wa mazishi ya Rais Mstaafu hayati Daniel arap Moi.

Wanamitandao hao walidai kimzaha kuwa, ni kupitia kwa kuitwa kwa na kiongozi huyo ambao kulisababisha kuachiliwa kwake kizuizini.

You can share this post!

Rungu la Moi sasa launganisha ‘vitoto vya kifalme’...

‘Tumieni Valentino Dei kuzuru hifadhi ya...

adminleo