• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
‘Marufuku hii inamaanisha nitalala njaa kwa siku 21’

‘Marufuku hii inamaanisha nitalala njaa kwa siku 21’

NA RICHARD MAOSI

Marufuku ya raia kutoingia na kutoka jijini Nairobi, yamepokelewa kwa hisia mesto miongoni mwa wakazi wa kaunti ya Nakuru na viunga vyake.

Hii ni baada ya rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumatatu kutangaza rasmi kuwa shughuli za usafiri katika kaunti nne ambazo ni Kwale, Mombasa, Kilifi na Nairobi zisitishwe, katika mchakato wa kukinga raia dhidi ya mkurupuko wa homa ya Covid-19.

Francis Nderitu ambaye ni dereva wa matatu ya 2NK Sacco kutoka Nakuru -Nairobi anasema hatua yenyewe itamfanya akose riziki ya kila siku.

“Wengi wetu tumekuwa tukipata riziki yetu mjini Nairobi, kwa kusafirisha abiria na wakati mwingine mizigo. Marufuku hii inamaanisha nitalala njaaa kwa siku 21,” akasema.

Nderitu alieleza kuwa afadhali serikali ingetoa ilani ya siku nne au wiki moja, ili kuwapatia wafanyibiashara na madereva muda wa kutosha kujiandaa kabla ya kuanza kutekeleza agizo la serikali.

Wakati wa mazungumzo ya kipekee na Taifa Leo Dijitali kwa njia ya simu, Bw Nderitu alikuwa amekwamia jijini Nairobi baada ya mipaka ya kutoka kufungwa mara moja, na maafisa wa usalama.

Aidha alieleza hatua hiyo ingemtenganisha na familia yake changa ambayo inakaa mtaani Shaabab kaunti ya Nakuru.

Lakini Amos Omanga ambaye ni dereva wa Solai Sacco amepokea agizo la rais kwa mikono miwili akisema ni njia dhabiti ya serikali kuwakinga wananchi wanaopatikana katika kaunti zingine.

Alisema kuwa siku 21 zinatosha kuwatambua wale wanaogua maradhi ya Covid -19, kisha wakatengwa na kutibiwa.

“Ninawaomba madereva wenzangu kutii sheria, kwa sababu sio jambo rahisi kushindana na serikali,”aliongezea.

Amri yenyewe inajiri wakati ambapo safari za reli, ndege na barabarani zimepigwa marufuku hii ikiwa ni mikakati ya serikali kuu kuzuia mkurupuko wa maradhi ya Covid-19.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali kamishna  wa Bonde la Ufa George Natembeya alidokeza kuwa polisi watahakikisha kuwa mianya yote ya kuingia na kutoka Nairobi imezibwa tayari.

Mikakati yenyewe inalenga kuhakikisha abiria hawatasafiri kutoka Nairobi kuingia Nakuru isipokuwa wasambazaji wa bidhaa muhimu kama vile vyakula.

Wengine waliounga mkono agizo la rais ni gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui na mwenzake wa Machakos Alfred Mutua.

  • Tags

You can share this post!

‘Nilikuja Australia kutazama mbio za magari ya...

Ndingi alipouza ‘Benz’ yake kununulia watu ardhi

adminleo