Masaibu zaidi yamwandama Gavana Waititu
Na KIPCHUMBA SOME
Baada ya madiwani kumvua wadhifa, Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu ameanikwa zaidi baada ya kubainika kuwa familia yake ilifaidi kwa zabuni ya Sh20 milioni katika serikali kinyume na sheria.
Kulingana stakabadhi ambazo Taifa Jumapili iliweza kuona, kampuni tano zinazomilikiwa na mkewe Waititu, Bi Susan Wangari Ndung’u na binti zake; Monica Njeri Ndung’u na Diana Wangoko Ndung’u zilifanya biashara ya thamani ya Sh18,871, 398 kati ya Oktoba 2017 na Machi mwaka huu.
Kampuni hizo ni Suwanga Ltd, Modiba Ltd, Beedee Management Services Ltd, Connex Logistict Ltd na Bin Management Ltd.
Kampuni tatu kati yazo, zilisajiliwa baada ya Bw Waititu kuingia mamlakani ilhali moja alisajiliwa miezi miwili kabla ya mwanasiasa huyo kuchaguliwa kuwa gavana. Bin Management Ltd ilisajiliwa mnamo 2010.
Bw Waititu hakujibu simu zetu tulipomtaka kuzungumzia suala hilo, ambalo linaonyesha wazi alitumia mamlaka ya afisi yake kufaidi familia yake.
Mnamo Alhamisi, alitutumia ujumbe mfupi akisema: “Jaribu upate maelezo zaidi na ushahidi tosha.”
Hatua ya serikali ya Kiambu kuzipa kampuni zinazomilikiwa na watu wa familia ya Waititu zabuni inakwenda kinyume na sehemu ya 66 (8A) ya Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Bidhaa za Umma 2015.
Sehemu hiyo inasema: “Mtu au jamaa za mtu wanapopewa zabuni katika asasi anayosimamia atakuwa, ametenda kosa kwa mujibu wa sheria ya ununuzi na uuzaji bidhaa.”
Ufichuzi huu mpya huenda ukaongeza presha kwa Bw Waititu ambaye anakabiliwa na kesi za ufisadi na matumizi mabaya ya afisi yake, pamoja na mkewe, kuhusiana na zabuni ya kima cha Sh588m.
Kuweka msumari moto kwenye kidonda, Ijumaa madiwani walipitisha hoja ya kumwondoa afisini.
Isitoshe, Mahakama ya Rufaa ilidumisha uamuzi wa Mahakama Kuu ulioagiza kwamba Bw Waititu na magavana wengine wawili wanaokabiliwa na kesi za ufisadi wazuiwe kuingia afisini zao hadi kesi hizo zitakaposikizwa na kuamuliwa.
Kulingana na stakabadhi katika afisi za msajili wa kampuni, kampuni ya Suwanga Ltd iliyopewa zabuni ya thamani ya Sh3,999,835, ya ujenzi wa choo, mnamo Januari 30, 2018 ilisajiliwa mnamo Juni 9, 2017, miezi miwili kabla ya Waititu kuingia afisini. Na ikalipwa kwa kazi hii baada ya ujenzi huo kukamilika.
Stakabadhi hizo zinaonyesha kuwa Bi Susan Wangari Ndung’u ndiye mmiliki wa kipekee wa kampuni hiyo.
Nayo kampuni ya Modiba Management Services Ltd ilipewa zabuni ya kuwasilisha magurudumu 30 ya thamani ya Sh874,000 mnamo Novemba 29,2017.
Kampuni hiyo iliwasilisha bidhaa hizo mnamo Desemba 6, 2017 na ikalipwa siku hiyo, kulingana na vocha za malipo tulizoweza kuona. Modiba Management Services Ltd ilisajiliwa mnamo Novemba 1, 2017 kwa jina la Monica Njeri Ndung’u ambaye ni bintiye Bw Waititu.