• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Maseneta wamlaumu Gavana Wambora kuhusu usimamizi wa fedha za umma

Maseneta wamlaumu Gavana Wambora kuhusu usimamizi wa fedha za umma

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Embu Martin Wambora Alhamisi alikuwa na wakati mgumu mbele ya maseneta alipotakiwa kueleza ni kwa nini serikali ilifeli kutumia Sh358 milioni za maendeleo katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018.

Hii ni baada ya ripoti ya aliyekuwa Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Edward Ouko, kubaini kuwa pesa hizo zilikuwa kwenye akaunti ya serikali hiyo kufikia Juni 20,2018.

Wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu na Uwekezaji (CPAIC) pia walimlaumu gavana Wambora baada ya kubainika kuwa serikali yake ilikusanya mapato ya Sh532 milioni mwaka huo ilhali ililenga kukusanya Sh892 milioni.

“Kwa kukosa kutumia Sh358 milioni, hii ina maana kuwa serikali yako iliwanyima wakazi wa Embu maendeleo ambayo tayari ilikuwa imepangiwa. Hili ni kosa ambalo linastahili adhabu kubwa, kwani sisi kama maseneta tunapigania nyongeza ya fedha kwa kaunti ilhali wewe hapa hauzitumii kwa miradi iliyokusudiwa,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo Sam Ongeri.

Bw Wambora alilkuwa amefikia mbele ya kamati katika ukumbi wa Shimba Hills, jumba la KICC, Nairobi kutoa majibu na ufafanuzi kuhusu hitilafu zilizoibuliwa kwenye ripoti ya Bw Ouko kuhusu matumizi ya fedha za umma Embu mwaka wa kifedha wa 2017/2018.

Akijitetea Gavana huyo ambaye alikuwa ameandamana na maafisa wakuu katika serikali yake, serikali yake iliyokosa kutumia Sh358 milioni kwa sababu pesa hizo ziliwasilisha kutoka Hazina ya Kitaifa kuchelewa.

“Isitoshe, mitambo ya usimamizi wa fedha kielektroniki (IFMIS) ilikuwa na hitilafu. Lakini hata kama IFMIS ilikuwa sawa bado hatungetumia fedha hizo kwa sababu ziliwasilishwa mwezi wa Julai, 2018 ilhali zinapasa kufikia kabla ya Juni 30, 2018,” Bw Wambora akasema.

Hata hivyo, hakueleza ni kwa nini pesa hizo zilijumuishwa katika taarifa ya kifedha ya mwaka wa kifedha wa 2017/2018 ilihali ziliwasilishwa baada ya kutamatika kwa kipindi hicho.

“Kwa nini basi pesa hizo zikajumuishwa katika ripoti ya kifedha iliyowasilishwa kwa wakazi wa hesabu katika mwaka huo. Hii ni makossa na inaonyesha kuwa maafisa katika idara ya fedha kaunti ya Embu hawaelewi majukumu yao,” akasema Seneta wa Isiolo Fatuma Dullo.

Kuhusu kufeli kukusanya mapato kama ilivyokadiriwa katika bajeti ya Embu, Bw Wambora alijitetea kwa kusema kuwa hali hiyo ilichangiwa na joto la kisiasa wakati huo ikizingatiwa kuwa ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi mkuu.

“Hali ya mshike mshike iliyotokana na kampeni za kisiasa ndio iliathiri uwezo wetu kukusanya mapato. Lakini hali hiyo iliimarika baada ya uchaguzi huu,” akasema Bw Wambora.

Hata hivyo, Seneti wa Embu Njeru Ndwiga alipuuzilia mbali maelezo hayo akisema machafuko ya kisiasa hayakushuhudiwa katika kaunti ya Embu, yaliyokuwa katika sehemu kama Nairobi.

“Sikubaliani na wewe Bw Gavana. Hatukuona mawe yakirushwa Embu na watu wakifunga maduka. Binafsi niliendesha kampeni zangu katika mazingira matulivu,” akasema Ndwiga.

  • Tags

You can share this post!

Ligi ya Japan yakosa kisa cha corona

Kaunti zote zitapokea fedha Jumatatu – Serikali