• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Maseneta wapinga mpango wa kupigwa marufuku kwa mbolea ya kiasili

Maseneta wapinga mpango wa kupigwa marufuku kwa mbolea ya kiasili

 

Na CHARLES WASONGA

MASENETA wamepuuzilia mbali pendekezo la kuharamishwa kwa matumizi ya mbolea aina ya samadi isiyokauka katika ukuzaji wa mimea ya chakula, wakisisitiza kutoruhusu utekelezwaji wa pendekezo hilo.

Maseneta hao walionekana wenye hasira Jumanne walisema pendekezo hilo lililotolewa na idara ya afya ya mimea limeleta kero kubwa katika sekta ya kilimo haswa wakulima wenye mashamba madogo.

Walitaja mbolea asili kama ambayo ndiyo bora katika enzi hizi huku wakisema kuwa kununi hizo zilizotungwa na wizara ya kilimo zitaathiri zaidi sekta ya kilimo nchini.

Hata hivyo, kanuni hizo hazijawasilishwa katika bunge ili yajadiliwe na kuidhinishwa au kukataliwa.

“Inasikitisha kuwa mtu anaweza kupinga matumizi ya mbolea ya kiasili wakati huu. Wakulima wamekuwa wakishauriwa kupunguza matumizi ya mbolea ya kisayansi kwa kutokana na athari zake shambani,” akasema Seneta wa Uasin Gishu Profesa Margaret Kamar.

Suala hilo liliibuliwa wakati wa kikao cha alasiri cha Seneti na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.

Seneta huyo ambaye ni kiongozi wa Ford Kenya aliitaka serikali ya kitaifa kuelezea mantiki ya pendekezo hilo la kupiga marufuku matumizi ya mbolea ya samadi isiyokauka.

“Inadaiwa kuwa marufuku hayo yanalenga kuwanufaisha kampuni kubwa kimataifa ambazo hutengeneza mbolea ya kisasa na wauzaji bidhaa hizo humu nchini. Huku watu hawa wakifaidi walima watakuwa wakipata hasara,” akasema Bw Wetang’ula.

Hata hivyo, Wizara ya Kilimo ilisema kuwa kanuni hizo zinalenga kuhakikisha kuwa mazao ya chakula humu nchini ni salama ili kuweza kukubalika katika masoko ya ng’ambo.

You can share this post!

MAUAJI YA WANGECHI: Daktari mtarajiwa alikuwa mwerevu...

Wamalwa asema hali ya ukame sio mbaya nchini

adminleo