• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Maseneta wawapongeza Uhuru na Raila kwa kuokoa jahazi

Maseneta wawapongeza Uhuru na Raila kwa kuokoa jahazi

NA CHARLES WASONGA

MASENETA Alhamisi jioni walimwamiminia sifa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Rais Odinga kwa kuwawezesha kuelewana kuhusu mfumo mwafaka wa ugavi wa fedha baina ya kaunti.

Wakishiriki katika mjadala kuhusu suala hilo, maseneta wa mirengo mbili pinzani waliungama kuwa ahadi ya Rais kwamba kaunti zitaongezewa Sh53.5 bilioni mwaka ujao ndio ilimaliza mvutano huo.

Kwa muda wa miezi mitatu iliyopita, maseneta wote 67 wamekuwa wakivutana baada ya 25 miongoni mwao,  kupinga mfumo ambao ungechangia kaunti 18 kupoteza jumla ya Sh17 bilioni. Waseneta hao wajibandika jina “Team Kenya”, kuashiria walitaka mfumo ambao ungeunganisha nchi.

Mfumo huo ambao ulikipa uzito kigezo cha idadi ya watu, ulipendekezwa na Kamati ya Seneti kuhusu Fedha inayooongozwa na Seneta wa Kirinyaga Charles Kibiru. Uliibuliwa kutoka kwa mfumo ambayo ulipendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) mwaka jana

Mfumo huo pia ulipendekeza nyongeza ya fedha kwa kaunti zenye watu huku ukipunguza mgao wa fedha kwa kaunti zenye zilizoko maeneo kame na pwani ya Kenya, ambazo ni kubwa kieneo japo zina idadi ndogo ya watu.

“Hatmaye leo (Alhamisi) tumeelewana kuhusu suala hili muhimu na ambalo tumejidili katika vikao 10 bila kwa miezi mitatu. Hii hasa imetokana hatua ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuingilia kati na kukubali kaunti ziongewe fedha mwaka ujao,” akasema kiongozi wa wengi Samuel Poghisio.

Kauli sawa na hiyo ilitolewa na naibu kiongozi wa wengi Fatuma Dullo, kiranja wa wachache Mutula Kilonzo Junior, seneta wa Kitui Enock Wambua miongoni mwa wengi.

Bi Dullo ambaye ni seneta wa Isiolo alisema alikuwa miongoni mwa maseneta walioalikwa katika mkutano katika Ikulu ya Nairobi ambapo Rais Kenyatta alitoa hadi hiyo ya nyongeza ya fedha kwa kaunti.

“Nashukuru Rais Kenyatta na Bw Odinga kwa kuingilia kati suala hili muhimu. Nilikuwepo katika mkutano huo na ningependa kuungamana kuwa ilikuwa ni siku yangu ya kwanza kuketi meza moja na Baba (Raila),” akasema huku maseneta wenzake wakicheka.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Ikulu Kanze Dena-Mararo baada ya mkutano huo wa Ikulu, ilisema kuwa serikali ilikubali kuziongezea kaunti Sh53.5 bilioni zaidi mwaka ujao, endapo uchumi wa nchi utaimarika.

“Mkutano huo umeafikia kulingana na hali ya uchumi utakavyokuwa, serikali itaziongezea serikali za kaunti Sh53.5 bilioni zaidi kutoka bajeti ya kitaifa,” taarifa ya Kanze ikaeleza.

Wakiongea na wanahabari katika majengo ya Bunge, Alhamisi jioni baada ya maseneta kukubaliona maseneta wanachama wa “Team Kenya” walitaja nyongeza hiyo kama ishara ya ushindi kwao.

Wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, walisema kuwa msimamo wao kuhusu suala hilo ndio ulisababisha Serikali Kuu kukubali kuongeza fedha kwa kaunti mwaka ujao.

“Tunafurahi kwamba kwa mara ya kwanza, seneti imefaulu kuisukuma serikali hadi ikakubali kuongeza fedha kwa serikali za kaunti. Kwa hivyo, sasa Wakenya wote wameshinda na kuibuka kuwa kitu kimoja,” akasema Bw Murkomen.

Seneta huyo wa Elgeyo Marakwet japo fedha hiyo zitatolewa mwaka wa kifedha wa 2021/2022, zitachangia pakuba maendeleo katika kaunti zote za humu nchini.

“Shule zaidi za chekechea, hospitali na soko nyingi zitajengwa katika kaunti zetu kwa manufaa ya watu wetu,” akasema Bw Murkomen ambaye alikuwa ameandamana na mwenzake wa Kakamega Cleophas Malala.

Bw Malala ambaye aliungama kuwa amedhulumiwa zaidi akipigania mfumo usiobagua kaunti zozote, alisema amewasamehe wale wote waliomdhulumu.

“Nafurahi kuwa sisi kama Team Kenya tumeshinda. Tumewashinda wale ambao walitaka kugawanya taifa hili kwa kupitia ugavi usio sawa wa rasilimali. Juzi niliangua kilio mbele yenu wanahabari lakini leo nacheka kwa furaha kwani hakuna kaunti itakayopoteza,” akaeleza.

Naye Seneta Wambua ambaye pia ni mwanachama wa Team Kenya sasa aliwataka magavana wote 47 kuhakikisha kuwa fedha za umma zimetumiwa vizuri kwa manufaa ya wananchi.

“Kama maseneta tumetekeleza wajibu wetu wa kupigania nyongeza ya fedha. Sasa kazi ni kwa magavana ambao ndio watasimamia fedha hizi; hatutaki kusikia visa vya fedha za umma kufujwa,” akasema Bw Wambua.

  • Tags

You can share this post!

Nyoro awahimiza wafanyabiashara kuunda vyama vya ushirika

Harambee Stars kupimana nguvu na Chipolopolo