Habari Mseto

Masharti makali yatolewa kulinda wanafunzi tamashani

August 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na IRENE MUGO

MABASI yanayosafirisha wanafunzi kuhudhuria mashindano ya kitaifa ya muziki yanayoendelea katika Kaunti ya Nyeri yatazuiliwa yakipatikana barabarani baada ya saa kumi na mbili jioni.

Kulingana na Mwenyekiti wa mashindano hayo, Bw Peter Wanjohi, walimu wa shule husika watahitajika kuwatunza wanafunzi wao ipasavyo.

“Shule zote zimepewa arafa inayotoa mwongozo kuhusu masharti haya. Sheria za trafiki zitatekelezwa na maafisa wa usalama watahakikisha sheria imefuatwa kikamilifu,” akasema.

Alitangaza hayo baada ya wanafunzi kumi kufariki kwenye ajali ya barabarani usiku wa kuamkia Jumapili.

Wachuuzi pia wamezuiliwa kuuza bidhaa zao katika Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi ambako mashindano hayo yanafanyika ili kuhakikisha wanafunzi hawapewi vyakula vitakavyodhuru afya zao.

Hatua hii pia imenuia kuzuia ulanguzi wa dawa za kulevya na pombe katika eneo hilo.

“Ili kuhakikishia wanafunzi wetu usalama, hatutaki kuona wachuuzi wakiingiza bidhaa zao hapa ndani,” akasema Bw Wanjohi. Maafisa wa afya ya umma katika kaunti wanatarajiwa kuchunguza maandalizi ya vyakula vyote vitakavyopikwa kwa ajili yawanafunzi hao 120,000.

Wakati huo huo, maafisa wa matibabu wamekita kambi katika chuo hicho endapo kutakuwa na matukio yoyote ya dharura yanayowahitaji.

Hii ni mara ya kwanza mashindano hayo kufanywa Nyeri na katika eneo la kati kwa jumla.

Katika tamasha hiyo kutakuwa pia na maonyesho kutoka kwa wanafunzi wa nchi za Rwanda na Sudan Kusini.

Maonyesho ya kwanza yalifanywa na wanafunzi wa chekechea na walemavu.

Kamishna wa eneo la kati, Bw Wilson Njenga, alihakikishia wanaohudhuria tamasha hiyo watadumishiwa usalama kwa wiki zote mbili.