Mashirika yataka Obado aendelee na kazi
Na IAN BYRON
MASHIRIKA ya kijamii katika Kaunti ya Migori yamewasilisha ombi kwa Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, ili aingilie kati na kusitisha mipango ya madiwani kumtimua Gavana Okoth Obado mamlakani.
ODM iliamua Bw Obado atimuliwe wakati aliposhtakiwa pamoja na watoto wake wanne kwa madai ya kufuja Sh73 milioni kutoka kwa kaunti hiyo.
Wakiongozwa na mratibu wa shirika la Nyanza Network Information Initiative Program aliye pia mwenyekiti wa Bunge la Wananchi tawi la Migori, Bw Peter Ogindi, walisema kumtimua Bw Obado kutarudisha nyuma maendeleo ya kaunti kando na kuibua taharuki ya kisiasa eneo hilo.
“Kiongozi wa chama anafaa kushauri viongozi wabadili msimamo kuhusu kumng’oa Gavana Obado mamlakani. Tayari tunashuhudia taharuki tele na zinaweza kusababisha ghasia katika kaunti kwa hali itakayoathiri maendeleo,” akasema Bw Ogindi.