Maskwota walia kutelekezwa na serikali ya kaunti
NA KALUME KAZUNGU
MGOGORO unazidi kutokota kati ya serikali ya kaunti ya Lamu na wakimbizi wa ghasia za Shifta eneo hilo kufuatia kile wanachodai kuwa ni kutelekezwa na utawala wa kaunti hiyo katika kupata haki yao ya kumiliki ardhi.
Mnamo 1964, maelfu ya wakazi wa vijiji vya Ishakani, Kiunga, Mwambore, Rubu, Simambaye, Mvundeni, Ashuwei, Matironi, Mkokoni,Vumbe, Saadani, Kiangwe, Ndhununi na Bodhei, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki walilazimika kuvunja nyumba zao na kuhamia maeneo salama, ikiwemo kisiwani Lamu na nje ya kaunti hiyo, ikiwemo Kilifi, Mombasa na hata nchi jirani ya Tanzania baada ya vita vya Shifta kukithiri eneo hilo.
Hali hiyo aidha imeathiri pakubwa maisha ya wakimbizi hao, ambao wengi wao mbali na kuwa maskwota wanaandamwa na ufukara mkubwa.
Katika kikao na wanahabari mjini Lamu Alhamisi, wakimbizi hao waliilaumu kaunti kwa kutowajibikia suala tata la ardhi hasa kwa maskwota hao wa Shifta.
Wakiongozwa na Msemaji wao, Mohamed Mbwana, walisema hawajaridhishwa na hali ambapo ardhi na hatimiliki zimekuwa zikigawanyiwa wakazi wa sehemu mbalimbali za Lamu ilhali maskwota wa Shifta wakiendelea kutelekezwa na kuhangaika.
“Haturidhishwi na jinsi kaunti inavyotubagua. Sisi ndio maskwota wa kwanza kabisa nchini Kenya na tulitarajia kupewa kipaumbele katika ugavi wa ardhi na utoaji wa hatimiliki. Kwa nini watu wa Bar’goni, Hindi na sehemu zingine za Lamu wamepokea hatiumilikio ilhali sisi tumeachwa hivyo? Kaunti itende haki kwa wote,” akasema Bw Mbwana.
Maskwota hao pai waliishinikiza Tume ya Kitaifa ya Ardhi nchini (NLC) kuingilia kati na kuhakikisha suala zima la utoaji wa hatimiliki kwa maskwota wa Shifta linafaulishwa.
Bi Tima Amin alisema furaha yake ni kuona serikali ikiwakumbuka na kuwasaidia ili warejelee maisha yao ya kawaida.