• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Matakwa ya wazazi kabla ya shule kufunguliwa

Matakwa ya wazazi kabla ya shule kufunguliwa

Na VALENTINE OBARA

CHAMA cha wazazi kimetoa orodha ya mapendekezo ambayo kinataka yatekelezwe na serikali kabla uamuzi ufanywe kufungua shule.

Huku idadi ya maambukizi ya virusi vya corona ikionekana kupungua kwa siku kadhaa sasa, kumekuwa na mdahalo kuhusu uwezekano wa shule kufunguliwa kabla Januari mwaka ujao.

Katika kongamano kuhusu ugonjwa wa Covid-19 lililofanywa kupitia mtandao wa video jana, Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi nchini (KPA), Bw Nicholas Maiyo, alisema wazazi wanataka hakikisho kuwa watoto wao watakuwa salama kabla shule zifunguliwe.

Miongoni mwa mapendekezo aliyooroshesha ni kuwa serikali ipeane barakoa tano kwa kila mtoto, ihakikishe wanafunzi na wafanyakazi wanakaguliwa kiafya kabla kuingia shuleni na wawe na vyeti vya kuthibitisha hawajaambukizwa virusi vya corona.

Vile vile, wazazi wanataka shule ziwe zikinyunyiziwa dawa kila siku, watu wasiofaa kuwa shuleni wasiruhusiwe kuingia wakati wowote na kuwe na maji ya kutosha kila wakati shuleni kwa minajili ya kudumisha usafi.

Kulingana na Bw Maiyo, wazazi pia wanataka wasimamizi wa shule wahakikishe kuna maafisa wa matibabu shuleni, wafanyakazi wapewe mafunzo mwafaka kuhusu jinsi ya kutekeleza kanuni za kuepusha maambukizi ya corona, na maafisa wa afya wawe wakikagua shule kila mwezi.

Mwenyekiti huyo alisema jinsi ilivyo kwa sasa, itakuwa vigumu kufungua shule hivi karibuni.

“Hakuna miundomsingi ya kutosha kufungua shule kwa kanuni za kuepusha virusi vya corona. Madarasa ni machache ikilinganishwa na idadi kubwa ya watoto. Wazazi wengi pia hawana uwezo wa kugharimia mahitaji ya elimu ya watoto wao kwani hawana kazi,” akasema.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alikariri kuwa mkutano wa wadau utafanywa kabla uamuzi wowote kufanywa kuhusu kufungua shule.

Alikana kuwa wizara yake hutoa misimamo tofauti kuhusu ufunguzi wa shule, na kusisitiza msimamo umekuwa mmoja kwamba, janga la corona likidhibitiwa shule zitaweza kufunguliwa wakati wowote.

Wizara hiyo ilisema endapo shule zitafunguliwa, kila mtoto atahitajika kuwa na barakoa inayoweza kuoshwa na kudumu kwa miezi sita.

  • Tags

You can share this post!

Muthama aapa kuzima Kalonzo kisiasa 2022

Kesi zaumiza raia