Matatu zafungiwa nje ya katikati ya jiji, wakazi kuhangaika zaidi
Na VALENTINE OBARA
WAKAZI jijini Nairobi wanatarajiwa kukumbwa na hali ngumu ya usafiri Jumatatu Desemba 3 kufuatia tangazo la serikali ya kaunti kuwa kuanzia siku hiyo hakuna magari ya uchukuzi wa umma yatakayoruhisiwa kuingia katikati mwa jiji.
Kaimu Katibu wa kaunti hiyo, Bi Pauline Kahiga-Waititu, alisema mipangilio mipya iliyopitishwa Mei 2017 kupiga marufuku uegeshaji wa magari hayo katikati mwa jiji, itaanza kutekelezwa Jumatatu.
Hii inatokea wiki chache baada ya serikali kuu kupitia kwa Wizara ya Usalama wa Ndani kukaza kamba kuhusu utekelezaji wa sheria za barabarani, hali iliyosababisha uhaba wa magari ya uchukuzi wa umma kwa siku kadhaa nchini kote, na kulazimu wananchi wengi kutembea au kutumia hadi mara tatu ya nauli ya kawaida kwa safari zao.
“Notisi nyingine zozote za awali na barua zilizoidhinisha maeneo mengine kuwa vituo vya kupandisha au kushukisha abiria mjini zimefutiliwa mbali na hazitatambuliwa kisheria kuanzia siku ya Desemba 3, 2018,” akasema Bi Kahiga kwenye ilani iliyochapishwa kwenye baadhi ya magazeti.
Suala la kuhamisha magari ya uchukuzi wa umma kutoka katikati mwa jiji limekuwa likijaribu kutekelezwa kwa miaka mingi sasa, lakini hugonga mwamba kila wakati.
Hii hutokana na malalamishi ya wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma pamoja na baadhi ya wakazi kuhusu hali mbovu ya vituo ambavyo magari hayo huhamishiwa.
Vituo hivyo vipya pia ni vidogo mno, na pia viko mbali kutoka katikati mwa jiji ilhali hakuna magari ya kuingiza wakazi mjini. Bodaboda pia zimepigwa marufuku kuingia jijini.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo jana, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Matatu (MOA), Bw Simon Kimutai alisema serikali ya Kaunti ya Nairobi haikushauriana nao kabla ya kutoa ilani hiyo.
“Tumeiona ilani hiyo kwenye vyombo vya habari. Kila mara tukizungumza kuhusu suala hili, huwa inaishia kuwa majibizano tu, kwa hivyo wakati huu hatutasema chochote. Watu wasubiri waone kutakavyokuwa Jumatatu,” akasema. Bw Kimutai
Uongozi wa Gavana Mike Sonko unataka magari yanayotumia barabara ya Waiyaki, Thika, Uhuru Highway, Kipande na Limuru kukamilisha safari zao katika kituo cha Fig Tree.
Magari ya barabara ya Jogoo yatahitajika yatatakiwa kutamatisha safari Muthurwa, yale ya Ngong yasimame Railways, ya Lang’ata na Mombasa Road yasimame Hakati, na yale yanayotoka maeneo ya bara yasimame katika kituo cha magari cha Machakos.
Magari pekee ambayo yatakuwa yakipitia mjini ni yale yanayotoka katika mitaa mbalimbali yakienda moja kwa moja hadi Upper Hill na kurejea.