Matayarisho kabambe yastahili kabla shule zifunguliwe – mbunge
Na LAWRENCE ONGARO
MIKAKATI maalum inastahili kuwekwa na serikali kabla ya kufunguliwa kwa shule kote nchini, amesema mbunge.
Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema mipango kadha inastahili kuzingatiwa kwanza kabla ya kuwaruhusu wanafunzi kurejea shuleni.
“Tunaelewa vyema homa ya corona imesababisha mambo mengi kusimama na kwa hivyo kabla ya masomo kurejelewa ni vyema washika dau wa sekta ya elimu waje pamoja na mikakati itakayokuwa mwafaka kwa kuruhusu masomo kurejelewa jinsi inavyostahili,” alisema Bw Wainaina.
Alisema cha muhimu ni kuhakikisha shule zinakuwa na maji kwa wingi katika matangi na vyoo pia vijengwe vya kutosha.
“Wakati huu wakuu wa shule watalazimika kuwa mstari wa mbele kuhakikisha baadhi ya mabadiliko yanayopendekezwa yanafuatwa vilivyo. Maagizo yote ya Wizara ya Afya ni sharti yafuatwe jinsi inavyostahili ili kufanikisha mapendekezo hayo,” alisema mbunge huyo.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jana katika afisi za NG-CDF mjini Thika alipohutubia waandishi wa habari akitoa maoni yake.
Alisema kwa zaidi ya miezi mitano kupitia hazina ya fedha za maendeleo NG-CDF ameweza kukarabati zaidi ya shule 20 na kuweka matangi ya maji ya uwezo wa ujazo wa lita 10,000 kwa kila moja.
Alisema shule nyingi za msingi katika eneo la Thika zimefanyiwa ukarabati ambapo wanafunzi wakirejea masomoni watapata mazingira mapya.
Alipongeza mpango wa serikali wa kutoa Sh1.9 bilioni za kuunda madawati yatakayosambazwa katika shule kadhaa nchini.
Kutokana na mpango huo madawati 650,000 inatarajiwa yataundwa katika karakana za juakali.
Alipendekeza kuwa serikali iwape nafasi wanafunzi wa daraja la 5 hadi 8 nafasi ya kurejea kwanza shuleni, kabla ya madarasa ya nchini kurejea.
Alisema hali ya masomo itabadilika kwa sababu kulingana na pendekezo la serikali madarasa mengi yataruhusiwa kuwa na wanafunzi nchini ya 20, ikilinganishwa na hapo awali yalivyokuwa na wanafunzi 70.