Matiang'i afanya mabadiliko katika utawala wa mkoa
Na CHARLES WASONGA
WAZIRI wa Usalama Fred Matiang’i amewahamisha makamishna 15 wa kaunti na kuteua wengine sita katika mabadiliko aliofanya katika utawala wa mkao.
Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumatano, Waziri Matiang’I pia aliwapa uhamisho manaibu 98 wa kamishna na wengine wapya 84.
Alisema mabadiliko hayo yalifikiwa baada ya mashauriano na Rais Uhuru Kenyatta.
Katika Wizara ya Masuala Ndani Moffat Kangi na Wilson Njenga walietuliwa katika wadhifa wa Katibu Mkuu Mwandamizi na Katibu wa Idara ya Usalama wa Ndani, mtawalia.
Mshirikisha wa Ukanda wa Magharibi Anne Ngetich amehamishwa hadi Afisi ya Rais huku mwenzake wa Nyanza James Kianda akihamishwa hadi Nairobi kujaza nafasi ya Njenga.
Magu Mutindika na Esther Maina wameteuliwa kuwa Washirikishi wa Kanda za Nyanza na Magharibi, mtawalia.
Makamishna wa Kaunti pia wamehamishwa katika mabadiliko hayo.
Kamishna wa Kaunti ya Marsabit Evans Achoko amehamishwa hadi kaunti ya Kajiado kwa wadhifa huo huo huku Michael Tialal akihamishwa kutoka Siaya hadi Garissa ambako ataendelea kuhudumu kama kamishna wa kaunti.
Kamishna wa kaunti ya Mombasa Gilbert Kitiyo amehamishwa hadi Mandera, huku Stephen Kihara akiondolewa kaunti ya Kisii na kupelekwa kaunti ya Uasin Gishu.
Kamishna wa kaunti ya Garissa Mwangi Meru amehamishwa hadi kaunti ya Narok; George Omoding akihamishwa kutoka Bomet hadi Nandi; Samuel Kimiti akihamisha kutoka Narok hadi Bungoma.
Wengine sita wameteuliwa kuwa Makamishna wa Kaunti.
Wao ni pamoja na; Fredrick Ndunga (Machakos), Paul Rotich (Siaya), Mathias Mbogai (Tana River), Moses Lilan (Homa Bay), Benson David (Nyandarua) na Josephine Ouko (Bomet).