Matiang'i aongoza sherehe ya kumuaga Boinnet
Na CHARLES WASONGA
SERIKALI Ijumaa jioni iliandaa sherehe ya kuamuaga rasmi aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet.
Kulingana na taarifa kutoka kwa Wizara ya Usalama wa Ndani na Ushirikishi wa Majukumu ya Serikali ya Kitaifa, sherehe hiyo ilifanyika katika Hoteli ya Intercontinental, Nairobi kuanzia saa kumi na mbili na nusu jioni hadi saa tatu usiku.
Baadhi ya maafisa wa serikali wa ngazi ya juu walikuwa pamoja na Waziri wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i, Katibu wake Dkt Karanja Kibicho, Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti miongoni mwa wengine.
“Dkt Matiang’i alikuwa miongoni mwa maafisa wa serikali waliohudhuria sherehe ya kuamuaga Joseph Boinnet katika mkahawa wa Intercontinental, Nairobi. Aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi sasa ni Waziri Msaidizi katika Wizara ya Utalii na Wanyama Pori,” Wizara ya Masuala ya Ndani ikasema kwenye taarifa katika ukurasa wake wa Twitter.
Sherehe hiyo iliandaliwa miezi miwili baada ya Boinnet kuteuliwa kuwa Waziri Msaidizi (CAS) katika Wizara ya Utalii na Wanyamapori inayoongozwa na Waziri Najib Balala.
Muhula wake wa kuhudumu katika Idara ya Polisi ulikamilika mnamo Aprili 20, 2019.