Matibabu ya bure katika hospitali ya Matiba
Na NDUNGU GACHANE
FOLENI ndefu zinaendelea kushuhudiwa katika Hospitali ya Macho na Meno ya Kenneth Matiba tangu kufariki dunia kwa mwanasiasa huyo.
Hali hiyo inatokana na tangazo la Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria kwamba hospitali hiyo ya ghorofa nne, inatoa matibabu maalum ya bure kwa wakazi, ili kumuenzi mwanasiasa huyo mpiganiaji ukombozi wa pili anayefanyiwa mazishi Alhamisi.
Tangu Jumanne wiki jana, wagonjwa wamekuwa wakifika mjini Kenol kwenye barabara ya Nairobi-Nyeri, baadhi wakisafiri kutoka Lamu, Garissa na Nyandarua miongoni mwa kaunti zingine.
Kelvin Mukhwaya, mkazi wa Kaunti ya Siaya ambaye alikuwa na matatizo ya macho baada ya kudungwa na waya ni mmoja wa walionufaika kutokana na huduma hizo za bure.
Bw Mukhwaya alidungwa alipokuwa akitengeneza ua ambapo alikimbia katika hospitali iliyokuwa karibu. Alipewa dawa iliyozidisha maumivu yake.
Marafiki zake walimpeleka katika Hospitali ya Kenneth Matiba ambako alipokelewa katika eneo la wagonjwa wa dharura.
Alifanyiwa upasuaji ili kurekebisha jicho hilo lililokuwa limejeruhiwa vibaya katika ajali hiyo.
“Jicho langu lilikuwa limefura na lilikuwa karibu kutolewa kwa sababu nilipoenda katika kituo cha matibabu walinipa dawa ya maji ambayo ilizidisha hali,” alisema.
“Lakini hatua ya dharura ya madaktari iliniokoa. Nimefurahi sana kwa sababu sikutakiwa kulipia huduma hiyo,” aliongeza.
Kulingana na Gavana Wairia, hospitali hiyo ya Sh100 milioni inatoa huduma za bure kwa heshima ya marehemu Matiba ambaye ni shujaa wa kitaifa. Matiba alidhulumiwa alipokuwa akitetea wananchi dhidi ya uongozi wa chama kimoja.
Kwenye mahojiano Jumatatu, Bw Wairia alisema tangu hospitali hiyo ilipoanzishwa mwaka mmoja na nusu uliopita, zaidi ya wagonjwa 400,000 wametibiwa macho na magonjwa yanayohusiana na macho na wengine 70,000 walio na matatizo ya meno wametibiwa.
“Hospitali ya sasa imo katika jumba la kukodishwa lakini tuko na ekari mbili katika kituo cha Kimorori ambazo tumetoa kwa ujenzi wa hospitali ya kudumu itakayogharimu Sh20 milioni,” alisema.
Kaunti hiyo imekuwa ikikodisha jumba ilipo hospitali hiyo, na mara kwa mara imeponea kufukuzwa.