MATUKIO 2019: Magenge ya vijana yaliteka Pwani nzima
Na MOHAMED AHMED na FADHILI FREDRICK
MAGENGE ya vijana wahalifu yamekuwa yakitatiza usalama katika ukanda wa Pwani hasa katika Kaunti ya Mombasa.
Visa vya wakazi kuvamiwa, kukatwakatwa kwa mapanga na kuporwa vimeripotiwa kwa muda sasa.
Mwaka wa 2019, hata hivyo utakumbukwa kwa kuwepo kwa visa vya magenge hayo ambavyo viligonga vichwa vya habari.
Ni katika mwaka huu ambapo nchi nzima ilijawa na hofu usiku wa Agosti 5 wakati vijana wahalifu walipovamia wakazi wa Bamburi na kuwakatakata kwa mapanga kabla ya kuwapora.
Taarifa zilianza kusambaa miongoni mwa wakazi hadi kwa Wakenya wengine kwenye mitandao ambapo sehemu ya Bamburi ilitajwa na kila mmoja katika wiki hiyo.
Wakazi 13 walivamiwa na kuumizwa vibaya na vijana hao ambao walikuwa wamebeba mapanga.
Ni tukio hilo ambalo lilipelekea Waziri wa Usalama wa Ndani, DKT Fred Matiang’i kufika kwa haraka katika Kaunti ya Mombasa na kutembelea eneo la Kisauni.
Kuja kwa Bw Matiang’i kulipelekea kuanzishwa vita dhidi ya mihadarati ambayo ilitajwa kuwa sababu kuu inayochangia kuchipuka kwa magenge hayo.
Kulingana na takwimu ya baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali, kaunti ya Mombasa inaongoza kuwepo kwa magenge hayo.
Hata hivyo, hata baada ya kutangaza vita na kutoa hakikisho ya kumaliza magenge hayo, visa vya watu kuvamiwa vimeripotiwa katika kaunti hiyo ya Mombasa.
Miongoni mwa walengwa zaidi wakawa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (TUM) ambao wanaoishi katika eneo bunge hilo la Kisauni.
Zaidi ya wanafunzi 10 walivamiwa na kuporwa ndani ya miezi miwili ya nyuma jambo ambalo lilipelekea wanafunzi hao kuandamana mnamo mwezi Novemba.
Siku chache baada ya maandamano hayo wakazi wengine 10 walivamiwa kwenye tukio lengine kama lile la mwezi Agosti.
Tukio hilo lilizua hofu baada ya kubainika kuwa ni genge jipya linalotambulika kama 86 Battalion ndio lilihusika katika shambulizi hilo la Novemba 24.
Kufuatia shambulizi hilo mshirikishi wa kanda ya Pwani John Elungata alisema kuwa kikosi maalum cha maafisa wa usalama kimeundwa ili kupambana na vijana hao.
“Tutajitahidi tuweze kupambana na vijana hao ili tuweze kuwa na siku kuu yenye amani,” akasema Bw Elungata.
Operesheni zilifuatwa na kupelekea kukamatwa kwa vijana zaidi ya 300 ndani ya muda huo huku wachache wakiuawa na polisi.
Wengi ya waliokamatwa ilibainika kuwa ni vijana wenye umri chini ya miaka 18 ambao tayari wameanza uhalifu.
Ni katika juhudi za polisi kupambana na megenge hayo yakiwemo yale ya Wakali Kwanza, Wakali Wao na Waliotengwa ndipo wanachama hao wakatorokea katika kaunti jirani.
Wakati wa siku kuu ya Jamhuri kaunti kamishna wa Kilifi Magu Mutindika alieleza kuwa wanachama wa genge la Waliotengwa sasa wanatekeleza uhalifu katika maeneo ya Mtwapa na Chumani.
Kutoroka kwa magenge hayo kumedhihirisha kazi kabambe inayotekelezwa na maafisa wa polisi kuyamaliza magenge hayo.
Hata hivyo, hofu bado ipo miongoni mwa wakazi wa Mombasa kwani visa hivyo bado vipo bado.
Ni matarajio ya wengi wakiwemo wakazi na wageni kuwa wakati tunapoingia mwaka 2020 magenge hayo yatakuwa yamezimwa.
Kwingineko, kaunti ya Kwale ilikuwa miongoni mwa kaunti za Pwani ambazo ziliathitika na mikasa ya kigaidi huku ikiwa idadi kubwa ya vijana waliojiunga na al-Shabaab na kuwa tishio la usalama kwa mashambulizi ya mara kwa mara.
Mnamo Machi, mwaka huuu maafisa wa polisi walivamia nyumba huko Ng’ombeni, ambapo washukiwa 10 wa Al-Shabaab walikuwa wamejificha na wakipanga njama kuanzisha shambulio katika kaunti hiyo.
Hata hivyo washukiwa hao walitoroka lakini polisi walifanikiwa kupata vitabu vya mafundisho ya kigaidi, vilipuzi, marungu, viatu na nguo za kijeshi.
Mnamo Agosti mtuhumiwa aliyedhaniwa gaidi aliuawa na polisi katika mapigano ys risasi katika kijiji cha Moshini huko Ng’ombeni.
Mtuhumiwa aliyetambuliwa kama Mohamed Rashid Mwatsumiro au jina la kiutani Msanii aliuawa katika nyumba yake wakati wa shambulio la polisi.
Kulingana na polisi mtuhumiwa huyo alihusidhwa na mauaji ya mzee wa kijiji Bakari Dondo na kiongozi wa dini ya kiislamu Bw Shee Fumbwe katika kijiji cha Mabokoni, kaunti ndogo ya Msambweni.
Huku serikali ikizindua njia tofauti za kiusalama kupambana na ugaidi, kunazo familia zinazolengwa kwa kudhaniwa kuwaficha wahalifu waliojiunga na al-Shabaab zinaishi kwa hofu kwa idadi ya watu wao wakitoweka kwa hali tatanishi na kutopatatikana.
Kesi kadha
Shirika la haki za binadamu, Haki Afrika mwaka 2019 pekee limeorodhesha kesi takribani 30 za mauaji na kupotea kwa vijana wanaoshukiwa kuwa magaidi.
Hivi majuzi familia ya Rashid Kombo, 20, iliomba polisi wamlete jamaa wao ambaye wanadai alikamatatwa na polisi kwa tuhuma za kuwa mshiriki wa kundi la kigaidi.
Bw Kombo, ambaye ni mwalimu wa madrassa katika kijiji cha Mulungunipa alisemekana alikamatwa na maafisa wa polisi.
Familia imewanyoshea kidole cha lawamamaafisa wa polisi kwa kushindwa kuwaelezea alipo jamaa yao.
Familia nyingine eneo la Ukunda ina huzuni kwa toweka kwa jamaa yao, Juma Said Sarai, 35. Familia inadai kwamba Bw Sarai alishikwa na kuwekwa ndani ya gari mnamo Oktoba 4, 2019, nyumbani kwao Kibundani na watu wanaoshukiwa kuwa maafisa wa polisi.
Kufikia sasa hajajulikana alipo licha juhudi za familia kumsaka.