Habari Mseto

Matumaini kwa raia maskini EU ikitoa Sh800m kuwasaidia katika utafutaji haki mahakamani

April 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA TITUS OMINDE

WAKENYA maskini wanaotafuta huduma za kisheria wamefaidika na ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) wa Sh850m.

EU ilitumia pesa hizo kama msaada kwa Wakenya wasiojiweza kumudu gharama ya kupokea huduma za haki kupitia mahakamani kupitia shirika la Huduma ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria (NLAS) nchini.

Afisa anayesimia maswala ya utawala na Uchumi, katika ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Alexandre Baron alisema mpango huo unalenga zaidi wananchi waliotengwa na walio katika mazingira magumu kupata huduma za mawakili ili kuhakikisha kesi zao zinafanyika katika mazingira shwari ya kupata haki.

Bw Baron alisema zaidi ya Wakenya milioni tatu hawawezi kumudu ada za kisheria na hivyo kufanya iwe vigumu kwao kupata haki ya viwango vya ubora hitajika.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa afisi ya NLAS North Rift katika mji wa Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu, alisema kuwa EU kupitia NLAS inalenga kuziba pengo kati ya wenye uwezo wa kifedha na wasiojiweza katika jamii katika juhudi za kupata haki.

“Lengo letu kuu ni kuimarisha upatikanaji wa haki miongoni mwa watu waliotengwa na walio hatarini katika jamii kwa nia ya kurejesha imani ya umma katika mfumo wa mahakama nchini,” alisema Bw Baron.

Bw Baron alisema kwamba EU imejitolea kuendelea kuunga mkono mahakama katika juhudi zake za kuimarisha upatikanaji wa haki katika maeneo ya mbali ya nchi kupitia Huduma ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria.

“Kuna haja ya dharura ya kuimarisha usawa katika upatikanaji wa haki miongoni mwa makundi yaliyo hatarini ikiwa tunatazamia kuwa na imani na mfumo wa mahakama,” aliongeza.

Bw Baron alitoa changamoto kwa serikali kuelekeza rasilimali zaidi kuelekea kwenye Huduma ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria katika kuhakikisha kuwa dira na dhamira yake inafikiwa kwa manufaa ya wananchi lengwa.

NLAS ilianzishwa mwaka 2016, chini ya Sheria ya Msaada wa Kisheria kupitia Sheria ya Mamlaka ya NLAS inajumuisha utetezi wa masuala yanayohusiana na haki za binadamu, upatikanaji wa haki miongoni mwa mahitaji mengine ya kisheria.

Bw Baron alifichua kuwa katika ushirikiano mpya na serikali, Sh5 bilioni zaidi zitatumika kuunga mkono juhudi za NLAS haswa kwa lenga asasi zianahusika na masweala ya haki zikiwemo polisi na idara za magereza.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa NLAS Fresiah Githumbi alisema zaidi ya Wakenya milioni saba bado wanakumbana na matatizo ya kisheria kuanzia ardhi, familia, uhalifu na ajira.

“Jambo la kusitikiza ni kwamba chini ya nusu ya idadi ya watu hawawezi kupata haki wakati wengine wanaishia kukata tamaa kwa sababu ya changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kulipa ada za mawakili na ada nyingine za kupata haki,” alisema.