Habari Mseto

Matunda ya Kazi Mtaani yaonekana mitaa kadhaa Nairobi

July 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

MPANGO wa kuhakikisha vijana wanajiendeleza kimaisha Kaunti ya Nairobi na maeneo mengine nchini unaendelea Kaunti ya Nairobi.

Mradi huo, Kazi Mtaani unalenga kupiga jeki kimapato vijana wasio na kazi na waliopoteza ajira kufuatia athari za Covid-19 nchini.

Aidha, unalenga wakazi wa mitaa ya mabanda mijini na pia mashambani.

Awamu ya kwanza ya mpango huo na iliyoshirikisha kaunti nane, zilizoathirika pakubwa na virusi vya corona, kulingana na Katibu Mkuu katika Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Mijini Charles Hinga ilianza na vijana 31,689

Kaunti hizo ni pamoja na Nairobi, Mombasa, Kiambu, Nakuru, Kisumu, Kilifi, Kwale, na Mandera.

Aidha, awamu ya pili ilianza mapema wiki hii, na inalenga zaidi ya vijana 270,000 katika kaunti zote 47.

Mitaa iliyoko pembezoni mwa Thika Superhighway, mpango huo ulizinduliwa na kuanza Jumanne, Julai 14, 2020, ambapo vijana waliobahatika kupata ajira walishiriki kufanya usafi wa barabara na mitaro ya majitaka.

Katika eneo la Zimmerman na Githurai, walifyeka nyasi kandokando mwa barabara na pia kukusanya taka.

“Tunashukuru Mungu na tunahimiza serikali iendelee kubuni nafasi za kazi kwa vijana. Wengi wetu hatuna ajira na tangu Covid-19 iingie nchini, maisha yamekuwa magumu,” akasema mmoja wa vijana hao.

Jumatano wameendelea na shughuli za kusafisha mitaa, chini ya mpango huo wa usafi wa kitaifa, NHP, na unaofadhiliwa na serikali kuu. Umetengewa kima cha Sh10 bilioni, kwa mujibu wa makadirio ya bajeti Mwaka wa Fedha 2020/2021 iliyosomwa Juni na Waziri wa Fedha Ukur Yatani.

Rais Uhuru Kenyatta alisema programu ya Kazi Mtaani inapania kusaidia vijana kupata nafasi za kazi kujikimu kimaisha, na walio kati ya umri wa miaka 18 – 36.

Mbali na kusafisha barabara na mitaro ya majitaka, kazi zingine watakazofanya ni kusafisha maeneo ya umma na pia njia.

“Tunalipwa Sh455 kwa siku,” kijana mwingine aliyepata nafasi hiyo ya ajira akaambia Taifa Leo.

Vifaa vya kazi vinatolewa na serikali za kaunti na pia kusimamiwa na maafisa wa kaunti na serikali kuu, wanaojumuisha vijana wa huduma kwa taifa ndio NYS.