MAUAJI YA KAMTO: Wito uchunguzi wa kina ufanywe
Na SAMUEL BAYA
VIONGOZI wa eneo la Pwani wamewataka polisi kuchunguza kwa kina mauaji ya aliyekuwa Naibu Gavana wa kaunti ya Kilifi, Bw Kenneth Kamto.
Bw Kamto alifariki baada ya kupigwa risasi tatu nyumbani kwake eneo la Nyali, Mombasa jana asubuhi.
Marehemu ambaye hadi kifo chake alikuwa mfanyabiashara jijini Mombasa alipigwa risasi hizo mbele ya mkewe sebuleni kabla ya kuaga dunia.
Maafisa wa polisi wakiongozwa na kamanda wa polisi eneo la Pwani, Bw Noah Mwivanda walithibitisha tukio hilo na kusema uchunguzi umeanzishwa.
Kufuatia kisa hicho, Gavana wa kaunti ya Kilifi, Bw Amason Kingi aliagiza bendera zote za serikali ya kaunti kuwekwa nusu mlingoti ili kumuomboleza Bw Kamto.
“Ni jambo la kusikitisha kwamba tumempoteza Bw Kamto na kama wakazi wa Kilifi, tumepoteza rafiki, ndugu na jamaa. Kwa sasa tunaitakia familia yake afueni wakati wakiendelea kuomboleza,” alisema Bw Kingi baada ya kuongoza viongozi wengine kutazama mwili wa marehemu katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali kuu ya mkoa wa Pwani
Aliongeza, “Na kwa sababu Bw Kamto alikuwa naibu wa kwanza wa Gavana wa kaunti ya Kilifi, pia nimeagiza bendera zote za serikali ya kaunti zipeperushwe nusu mlingoti kwa kumuenzi marehemu.”
Mkewe marehemu Bi Fauzia Kamto alieleza wanahabari kwamba mumewe aliingia mbio nyumbani mwendo wa tisa asubuhi.
“Jumanne jioni, mume wangu alikuja kunichukua kazini hadi nyumbani. Mimi ilipofika saa mbili jioni, nilienda hafla nyingine sio mbali sana na nyumbani na nilimuacha akiwa nyumbani bila tashwishi yoyote,” akasema.
Hata hivyo, aliporudi nyumbani mwendo wa saa tano usiku hakumkuta mumewe.
“Mimi niliangalia runinga lakini baadaye usingizi ulinizidi na nikalala kwa kiti. Hata hivyo, mwendo wa saa tisa asubuhi, mume wangu alifungua milango mbio akikimbilia jikoni. Wakati huo wote alikuwa akipiga kelele akisema niite askari mara moja,” akasema Bi Kamto.
Alisema muda mchache, majambazi watatu waliingia ndani hadi sebuleni. Mmoja wao aliichukua familia yote mateka huku mwengine akimfuata marehemu karibu na jikoni.
“Mume wangu alitoka tena jikoni lakini akikaribia sebuleni akapigwa risasi tatu.Muda huo wote, tulikuwa tumezuiliwa mateka na jambazi mmoja. Ninasikitika sana,” akasema mjane kabla ya kuanza kuangua kilio.
Viongozi wa eneo hilo waliendelea kutuma risala zao za rambirambi.
Wakiongozwa na naibu wa sasa wa gavana, Bw Gideon Saburi, walisema kifo hicho ni pigo kubwa kwa kaunti ya Kilifi.
Seneta wa Kwale Bw Issa Juma Boy,alitaka polisi wachunguze kifo hicho na kuwakamata washukiwa.
Aliyekuwa mbunge wa Kaloleni , Bw Gunga Mwinga pia alitaka chanzo cha mauaji hayo kichunguzwe.
Waliokuwa wabunge Gunga Mwinga(Kaloleni) na Anaina Mwaboza(Kisauni) pia waliomboleza kifo hicho cha Bw Kamto.
“Ni jambo la kusikitisha kwamba Bw Kamto alifariki katika kifo hiki. Hata hivyo ninaamini kwamba maafisa wa usalama watachunguza kiini hasa cha kifo hiki,” akasema Bw Gunga.
Seneta wa Kwale Bw Issa Juma Boy,ambaye ana uhusiano na familia hiyo alitaka polisi wachunguze kifo hicho na kuwakamamata wale ambao walihusika na uhalifu huo.
Mashirika ya kutetea haki za kibindamu ya MUHURI, Haki Africa na Tihuri pia yalitaka polisi wafanye uchunguzi wa haraka kuwakamata wale wote ambao wlaihusika na uhalifu huo.
“Ni wazi kabisa kwamba polisi wameshindwa na kukabiliana na ongezeko la utovu wa usalama katika kaunti ya Mombasa,” akasema Bw Francis Auma kutoka shirika la MUHURI.
“Mauaji haya sasa yanazidi kuthibitisha ukweli kwamba visa vya mauaji vinazidi kuwa kero katika kaunti ya Mombasa,” akasema Bw Husein Khalidi wa Haki Africa.
“Maafisa wa usalama lazima waanzishe mara moja uchunguzi kuhusu kifo cha Bw Kamto na kuwakamata wale wote ambao walihusika na uhalifu huo,” akasema Bw Eric Mgoja wa shirika la Tihuri.