Habari Mseto

Mauaji ya raia kiholela Samburu yazua tarahuki

June 16th, 2024 2 min read

NA MARY WANGARI

VIONGOZI katika Kaunti ya Samburu wameghadhabishwa na kulaani vikali ongezeko la visa vya mauaji ya kinyama yanayotekelezwa kiholela na watu wanaoshukiwa kuwa maafisa wa polisi.

Haya yamejiri baada ya mwanamme mmoja mchanga kupigwa risasi na kuuawa Alhamisi, Juni 13, 2024 mwendo wa saa nne asubuhi, katika eneo la Suguta, karibu kilomita 40 kutoka Maralal, Kaunti ya Samburu.

Wakihutubia wanahabari katika majengo ya Bunge Alhamisi, viongozi hao akiwemo Gavana wa Kaunti ya Samburu, Jonathan Lati na wabunge Lesuuda Naisula (Samburu Magharibi) na Dominic Letipila (Samburu Kaskazini) walikemea mtindo wa polisi kuchukua sheria mikononi mwao.

“Leo asubuhi tuliona maajabu, kitendo cha kinyama kabisa na tumeshangaa. Polisi walifika wakampiga risasi mguuni kijana mmoja na badala ya kumshika na kumpeleka kortini wakampiga risasi nyingine kichwani mbele ya kila mtu, machoni pa kina mama na watoto,” alieleza Gavana Lati.

“Askari walitaka kuonyesha nini kwa kumshurutisha mhasiriwa aketi na kisha kumuua hadharani. Mbona hawakumshika kama kweli alikuwa na hatia. Hakuwa na chochote, hakuwa na rungu wala bunduki.”

Kando na oparesheni ya kiusalama inayoendelea eneo hilo katika juhudi za kuzima majangili, ongezeko la visa vya mauaji ya kiholela yanayolenga raia limezidisha taharuki eneo hilo.

Kulingana na Mbunge Lesuuda, washambuliaji hao waliotorokea kuelekea Kaunti ya Laikipia, walifika kwa gari jeusi kabla ya kumpiga risasi na kumuua mhasiriwa na kumjeruhi mwendeshaji bodaboda aliyekimbizwa hospitalini,

“Wamekuwa wakiendesha oparesheni ya usalama na hamjawahi kutuona hata, lakini hatutawaruhusu waje wapige watu risasi mchana hadharani na kujeruhi wengine. Je, risasi hiyo ingekumbana na mtoto?” Alihoji Bi Lesuuda.

Viongozi hao sasa wanamtaka Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki na Inspekta Jenerali wa Polisi, Japhet Koome kuingilia kati suala hilo na kuwatia mbaroni wahusika.

Aidha, wameitaka serikali ya Rais William Ruto kutimiza ahadi yake kuhusu kukomesha mauaji ya raia kiholela yanayotekelezwa na maafisa wa polisi.

Mbunge Letipila alisema “oparesheni za kiusalama zinapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia sheria. Kama mtu anashukiwa kuhusu uhalifu wowote anafaa kukamatwa na kuwasilishwa kortini au kwa namna nyingine yoyote. Huwezi kumpiga mtu risasi hadharani na kujaza hofu jamii yote.

“Tunaunga mkono serikali katika oparesheni yake ya kiusalama katika juhudi za kurejesha utulivu maeneo ya Kaskazini mwa Kenya. Lakini kuna vipimo. Huwezi kumpiga risasi na kumuua hadharani mtu ambaye hajajihami.

Kisa hicho kimejiri siku chache tu baada ya kisa kingine ambapo watu wanaoshukiwa kuwa maafisa wa polisi walimuua kwa kumpiga risasi barobaro mmoja eneo la Rumuruti, Kaunti ya Laikipia.

“Tunajua hii ni serikali iliyosema hakutakuwa tena na visa vya watu kuuawa kiholela. Tunakumbuka wakati huo mwingine watu walikuwa wamejaza Mto Yala na mito mingineyo. IG asilale hadi ajue ni polisi gani wanaotaka kusawiri Kenya kama taifa lisilo na sheria,” alisema Gavana Lati.