Habari Mseto

Mavuno ya zaidi ya magunia milioni saba ya mahindi yanukia North Rift

Na EVANS JAOLA August 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WATAALAMU wa masuala ya kilimo Ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa, wametabiri kuwa eneo hilo litakuwa na mavuno tele msimu huu.

Hii ni kwa sababu ya kufanikiwa kuzima viwavi, kupatikana kwa mbegu za bure na hali shwari ya hewa.

Kupambana na wadudu waharibifu shambani kumesaidia mimea kunawiri huku wakulima wakiwa na matumaini ya mavuno mazuri.

“Mvua ambayo imekuwa ikishuhudiwa pia imesaidia kupunguza viwavi na wadudu wengi waharibifu ambao sasa hawawezi kuzaana,” akasema Mary Nzomo ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kilimo.

Idara ya kilimo imesema kuwa inatarajia mavuno ya zaidi ya magunia milioni saba ya mahindi msimu huu. Mapema mwaka huu, serikali ya Kaunti ya Trans Nzoia ilitumia Sh100 milioni kuwapa wakulima wadogo wadogo mbegu.

Idara ya Kilimo ya Kaunti ya Trans Nzoia pia ilisema wakulima wachache tu walilalamikia mashamba yao kuvamiwa na viwavi na wadudu wengine hatari.

“Mwaka huu hakuna malalamishi kwa sababu wakulima wengi pia mashamba yao hayakuathiri na wale ambao mashamba yao yalivamiwa, tuliwasaidia,” akasema Phanice Khatundi, Waziri wa Kilimo wa Kaunti ya Trans Nzoia.

Mapema mwaka huu, serikali ya kaunti ilisambaza mbegu ya mahindi kwa wakulima 258,000 kutoka 180,000 walionufaika mnamo 2024.