MAWAIDHA YA KIISLAMU: Kwa gharama hii, Ya Rabi ndiwe pekee wa kutunusuru
KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo. Leo hii tunamshukuru mno Maulana, Mola, Ya Rabi, Mwenye-Enzi-Mungu kwa kutujaalia kuwa hai.
Kwa neema hiyo ya kuwa hai, na kisha muhimu mno, kuwa waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu tunasema kwa kinywa kipana: Alhamdulillahi!
Ama tuchukue nafasi hii adhimu na adimu katika ukumbi huu kumshukuru mno Muumba wetu, mwenye kujaalia kila aina ya neema na rehema, ndiye pekee aliyeumba ardhi na mbingu na viumbe vyote vilivyomo. Anastahili yeye tu kuabudiwa, kuenziwa, kutukuzwa na kushukuriwa kwa kila aina ya shukrani.
Katika uzi uo huo, tunamtilia dua na kumfanyia kila aina ya maombi mwombezi wetu, Mtume (SAW). Sisi waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu tunafurahi, kumshukuru Mola kutujaalia kuwa hai na waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu. Atujaalie mwisho mwema Muumba wetu. Na awape maghofira wenzetu waliotangulia mbele za haki.
Ama ndugu yangu leo hii tunazidi kuwaombea nusra, afueni na amani ndugu zetu wanaokabiliwa na mitihani ainati. Si Sudan, Si Gaza, Si Ukraine, Si Jamhuri ya Kongo na kokote kule duniani. Adha na adhabu za binadamu zipo aina aina.
Ugumu wa maisha, gharama ya maisha, sio matozo ya ushuru, ughali wa bei za bidhaa na mitihani mingineyo mingi tu ya maisha.
Sasa hivi waja mbali mbali, na hasa wazazi wanaokabiliwa na ugumu wa maisha, wanapitia changamoto kadha wa kadha kutokana na karo, kodi na mitikisiko ya maisha.
Katika vyombo mbali mbali vya habari, waja wanalalama kuhusu kupanda kwa bei za bidhaa, kushindwa kumudu karo, kununua sare, vyakula na mahitaji mengineyo muhimu.
Si ajabu kuwa hadi sasa hivi baadhi ya wanafunzi, watoto wa matabaka mbali mbali hawajajiunga na shule kutokana na wazazi/walezi wao kushindwa kulipa karo. Ama hata kushindwa kununua vyakula na mahitaji mengine ya msingi.
Subhannallah!
Leo hii katika makiwanda mbali mbali, maabadi aina aina, misikiti, na kwingineko, ni wasaa mwafaka wa viongozi wa dini kujizatiti kuwatia shime na matumaini waja.
Maamuma wanakata tamaa kila kukicha. Allah (SWT) tujaalie tusikate tamaa. Aswailani tusikate tamaa. Daima, In Shaa Allah, tuishi na matumaini. Ipo siku.
Ni wakati muhimu huu kwa sisi waja kutiana moyo, kuhimizana na kusaidiana kwa hali na mali. Hali kama hii ya kusaidiana, kusemezana miongoni mwetu na kukinai kwa kidogo alichotujaalia Mola, itaepesha visa na mikasa, vurumai, mauji na dhiki tele katika jamii.
Hasa hasa vijana wetu wafunzwe kuwa na subira, wachapa kazi na wacha Mungu.
Taarifa za Imani, matumaini, kusaidiana zipewe kipaumbele majaaliwa katika vyombo vyetu vya habari. Inasikitisha kuona vijana wetu, baadhi yao, wakitumia njia za mkato kujichumia riziki na wanaishia pabaya!
Ya Allah (SWT) tujaalie maisha ya kheri na utuletea nusra katika maisha yetu, amina!
Ijumaa Mubarak