Habari Mseto

Mawakili maarufu wateuliwa kupunguza mrundiko wa kesi mahakamani

February 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Wakili maarufu Bw Otiende Amollo. Picha/ Maktaba

Na BENSON MATHEKA

MAWAKILI maarufu Otiende Amollo na Judy Thongori, ni miongoni mwa wapatanishi 180 waliosajiliwa na mahakama katika juhudi za kupunguza mrundiko wa kesi za kibiashara na kifamilia nchini.

Bw Omollo ambaye ni mbunge wa Rarieda, alisimamia ofisi ya kupokea malalamishi ya umma ilipoanzishwa chini ya katiba mpya, naye Bi Thongori ni mtetezi shupavu wa haki za wanawake.

Wapatanishi hao huteuliwa baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa na kamati ya mahakama ya upatanishi inayosimamiwa na Jaji Alnashir Visram wa Mahakama ya Rufaa.

Kwenye taarifa, kamati hiyo ilisema kufikia Januari 18 mwaka huu, ilikuwa imefaulu kuwasajili wapatanishi 180 kote nchini.

“Wapatanishi huchaguliwa kutoka wanaotuma maombi na kutimiza masharti yaliyowekwa na kamati. Mfumo wa kuwasajili huwa wa wazi na unaendelea,” ilisema taarifa ya kamati.

Kulingana na taarifa hiyo, kuna wapatanishi 99 wa kesi za kibiashara na 81 wa kushughulikia kesi za kifamilia. Baadhi ya mawakili ambao wamesajiliwa ni Maria Goreti Nyariki na Kyalo Mbobu.

Alipozindua mfumo huo mwaka jana, Jaji Mkuu David Maraga aliwakosoa mawakili kwa kutoukumbatia kikamilifu.

 

Kuathiri mapato

Alisema mawakili wanahisi kwamba mfumo huo ambao umefaulu kutatua kesi katika mahakama ya kusikiliza mizozo ya kibiashara na kifamilia utaathiri mapato yao.

“Mawakili ni kizingiti katika mfumo huu muhimu. Wanahisi kwamba mapato yao yatapungua iwapo mfumo huu utafaulu. Hata hivyo, ukweli ni kwamba una manufaa makubwa kwao kwani unapunguza muda na gharama ya kesi, kusaidia katika utafutaji wa haki na kujenga jamii yenye amani,” alisema Jaji Mkuu.

Aliongeza kwamba katika upatanishi, pande zote huwa washindi.

Tangu mfumo huo uanze kutumiwa, kesi katika mahakama ya kutatua mizozo ya kibiashara zimepungua kwa asilimia 50. Muda wa kusikiliza kesi pia ulipungua kwa siku 50.

Kupitia mfumo huo, mahakama imetatua kesi 25 na kuokoa zaidi ya Sh500 milioni kufikia mwaka jana.

Jaji Visram alisema wapatanishi huidhinishwa baada ya kukaguliwa na kuhojiwa vikali na kuna zaidi ya 400 waliotuma maombi na yanashughulikiwa.