Mawaziri wafisadi wa Uhuru wanavyoua Ajenda Nne Kuu
Na MWANDISHI WETU
JUHUDI za Rais Uhuru Kenyatta kutimiza ajenda zake nne kuu za maendeleo nchini kabla ya kustaafu mwaka 2022 zinazidi kupata pigo, baada ya baadhi ya mawaziri wake kuhusishwa na kashfa za ufisadi na kusababisha miradi mikubwa ya serikali kukwama.
Kukwama kwa mradi mkubwa wa unyunyiziaji maji wa Galana-Kulalu ambao ulilenga kuhakikisha kuna chakula cha kutosha nchini, ni mfano mzuri wa kufeli kwa waziri mhusika ambaye utepetevu wake umesababishia serikali kupoteza mabilioni ya pesa.
Tayari, mawaziri kadhaa wamefika mbele ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Mkuu wa Upelelezi (DCI) George Kinoti kuhusiana na madai ya ufisadi wiki hii.
Mnamo Jumatatu, Waziri wa Fedha Henry Rotich alihojiwa kuhusu madai ya Ufisadi katika ujenzi wa mabwawa mawili eneo la Bonde la Ufa na maafisa wa DCI, ambayo licha ya serikali kutoa zaidi ya robo tatu ya pesa za ujenzi, hakuna kazi muhimu ambayo imetekelezwa.
Tayari Waziri wa Maji Simon Chelugui amejitetea kuhusiana na sakata hiyo, akisema hajui lolote na kuwa tenda za ujenzi wa mabwawa hayo zilipotolewa hakuwa ameingia katika uwaziri.
Kwingineko, Waziri wa Utalii Najib Balala naye wiki hii alikuwa mbele ya tume ya EACC kuhojiwa kuhusu madai kuwa wizara yake ilitoa tenda ya Sh100 milioni kwa shirika la kitalii kutoka Amerika bila kufuata sheria.
Bali na Bw Balala, Bw Kinoti, aidha amekiri kuwa idara yake inapanga kumwalika Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri kufafanua kuhusu mzozo wa mbolea, ambapo serikali imekosa kuwapa wakulima mbolea ya bei nafuu.
Bw Rotich alirekodi habari kuhusiana na ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer ambayo yako katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, kwa gharama ya zaidi ya Sh65 bilioni.
Mabwawa hayo ni kati ya manne ambayo yako kwenye uchunguzi wa DCI, kuhusiana na madai ya ufisadi wakati wa kutolewa tenda, na kukwama kwa kazi katika maeneo yanapojengwa.
Matukio haya yanatendeka wakati Rais Kenyatta amewataka mawaziri kubeba msalaba wao wenyewe watakapopatikana na hatia.