• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mawaziri waidhinisha ardhi ya East African Portland iuzwe kulipa madeni

Mawaziri waidhinisha ardhi ya East African Portland iuzwe kulipa madeni

Na CHARLES WASONGA

KAMPUNI ya kutengeneza saruji ya East African Portland (EAPCC) imepewa idhini kuu ardhi yake ambayo haitumiki iuzwe  ili kupata fedha za kuisaidia kulipa madeni yake na kurejelea shughuli zake za kawaida.

Katibu wa Wizara ya Biashara na Viwanda Betty Maina Jumanne aliwaambia maseneta kwamba baraza la mawaziri limeidhinisha hatua hiyo ambayo itawezesha kampuni hiyo kupata Sh15 bilioni kutokana na mauzo ya ardhi yake na mali zingine.

Kampuni hiyo inahitaji kiasi hicho cha fedha ili iweze kulipa malimbikizi ya mishahara ya wafanyakazi, madeni ya Benki ya Kenya Commercial (KCB) na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Japan (JICA), kuifanyia ukarabati mitambo yake na kuwalisha wafanyabiashara walioiwasilishia bidhaa

“Taarifa ya Baraza la mawaziri kuhusu suala hili limetayarishwa na Wizara ya Fedha kwa ushirikiano na  ile Biashara na Viwanda.  Itawasilishwa katika baraza la mawaziri mwishoni mwa mwezi huu,” akasema Bi Maina.

Afisa huyo aliiambia kamati ya Seneti kuhusu Utalii, Biashara na Ustawishaji wa Kiviwanda kwamba kampuni hiyo inayomiliki mali ya thamani ya zaidi ya Sh100 bilioni haihitaji kunusuriwa na serikali.

Bi Maina alisema kile kampuni hiyo inahitaji ni kupewa ruhusa ili kutekeleza mikakati ambayo itaiwezesha kusaka fedha.

“Hatua hizo ni kama vile kuuza mali yake na kusaka mwekezaji wa kutegemewa,” Bw Maina akaiambia Kamati hiyo ambayo Jumanne iliyongozwa na Seneta wa Taita Taveta Johness Mwaruma.

Endapo kampuni hiyo itafaulu kupata pesa hizo, Sh15 bilioni, Bi Maina alisema, jumla ya Sh10.8 bilioni zitaelekezwa kulipa malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi na madeni mengine.

Kwa mfano, kampuni hiyo ambayo makao yake makuu yake katika eneo la Kitengela kaunti ya Kajiado, inadaiwa Sh4.2 bilioni na benki ya KCB.

Wale waliowasilishia bidhaa za matumizi pia wanaidai Sh2.6 huku wafanyakazi ambao walifutwa wanaidai Sh3.5 bilioni kama malimbikizo ya malipo ya kusimamishwa kazi.

Mkuregenzi Mkuu wa EAPCC Simon Ole Nkeri alisema kampuni hizo imepunguza uzalishaji wake kwa kima cha asilimia 50 kwa sababu mitambo yake imezeeka.

Mapema mwaka huu kampuni hiyo iliwafuta kazi jumla ya wafanyakazi 700, katika kile ilichosema ni juhudi zake za kuimarisha hali yake ya kifedha kwa kuipunguzia mizigo.

“Kampuni hii inahitaji Sh2 bilioni ili iweze kuzikarabati mitambo yake kutengeneza saruji kwa muda wa miezi miwili,” akawaambia maseneta.

Alisema kampeni hiyo ikiweza kurejelea shughuli zake za kawaida itaweza kupunguza gharama ya umeme ambayo wakati huu inaigharimu Sh120 milioni kwa wastani.

Bi Maina na Bw Ole Nkeri walikuwa wakitoa maelezo hayo kujibu baadhi ya maswali ambayo yaliulizwa na Seneta Maalum Judy Pareno.

Kimsingi, Bi Pareno alitaka maelezo kuhusu juhudi ambazo serikali inatekeleza kuhakikisha kuwa kampuni hiyo itaimarisha utendakazi wake na kuwalipa wafanyakazi waliofutwa malipo yao.

You can share this post!

MSWADA WA JINSIA: Mjadala waanza

Sonko awaita majambazi awape ajira

adminleo