'Mazao ya butternut ni mengi ila hayana soko'
Na SAMMY WAWERU
KILIMO ni uti wa mgongo wa Kenya na mataifa mengine Barani Afrika, ila kwa wakulima wa maboga madogo hawana sababu ya kutabasamu.
Hii ni kutokana na kuendelea kudorora na kukosekana kwa soko la zao hilo, maarufu kama butternuts.
Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Evaty Hawa na ambaye amekuwa mkulima wa malenge hayo kwa muda wa miaka kadhaa eneo la Machakos, amesema ana takriban tani 5 sawa na kilo 5,000 kwenye ghala.
“Kupata soko la butternuts imekuwa kibarua kigumu kwa wakulima, nina takriban tani tano kwenye ghala ambazo zimekosa wanunuzi,” akadokeza mkulima huyo, akishangaa atakakopeleka mazao hayo.
Kulingana na wakulima wenye uzoefu wa muda mrefu, ukuzaji wa maboga madogo ni rahisi na usio na gharama, hatua ambayo inachochea wakulima kuingilia kilimo chake.
“Gharama ya kuyazalisha ni ya chini sana. Isitoshe, ni rahisi kuyalima na yanatoa mazao ya kuridhisha, lakini kikwazo kikuu ni kupata soko.
“Wengi wanaendelea kuhangaika na mazao yaliyojaa kwenye maghala. Tunaomba serikali na wadauhusika, watusaidie kutatua changamoto za soko tupate wateja,” akasema Lenny Sylvester mtaalamu na mkulima wa butternuts Kaunti ya Siaya.
Kulingana na Bw Lenny, amekuza zao hilo mara mbili kwenye shamba lake, ila pandashuka za kupata wanunuzi nusra zimfishe moyo kuendelea.
“Nimesaidia wakulima kadhaa ambao ni wateja wangu kiushauri, maboga hayo yanapokomaa, malalamiko ni yaleyale mamoja; ukosefu wa soko,” akaelezea.
Huku soko la zao hilo likiendelea kuwa kero kikuu, wakulima wanahimizwa kukumbatia mfumo asilia kuyakuza.
“Butternuts zinaaminika kukuzwa kwa kutumia fatalaiza na dawa zenye kemikali kuzinawirisha na kukabili changamoto za wadudu na magonjwa, na ndio maana wengi wanahofia kuyala suala linalochangia kuharibika kwa soko. Ni muhimu wakulima wakumbatie mfumo wa kilimohai kuyazalisha,” anashauri James Murage, mtaalamu wa masuala ya kilimo.
Aghalabu, maboga hulishwa watoto sana, na mdau huyo anasema umewadia wakati wakulima kuepuka kutumia fatalaiza na dawa zenye kemikali, ili kuurejesha uhalisia wa zao hilo la zamani.
“Zamani, enzi za kina nyanya na babu, maboga madogo yalikuzwa kwa kutumia mboleahai, ile ya mifugo na hayakupuliziwa dawa. Yanayopuliziwa dawa, hunuka na kuwa na michirizi ya dawa. Ni hatari kwa walaji,” Bw Murage anaelezea.
Mbali na kurejelea na kukumbatia mfumo asilia kuyazalisha, wakulima pia wanahimizwa kufanya utafiti wa soko kabla kuanza kuyalima.