• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Mbinu anazotumia Raila kushinda uenyekiti AUC

Mbinu anazotumia Raila kushinda uenyekiti AUC

NA JUSTUS OCHIENG

WAZIRI Mkuu wa zamani Raila Odinga ameanza mchakato wa kuandaa mbinu ya kushinda wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) baada ya baraza kuu la umoja huo kumwondolea vizingiti katika ndoto yake ya kutwa kiti hicho.

Mkutano huo wa 22 wa Baraza Kuu la Mawaziri wa Mataifa wanachama wa Umoja wa Africa uliamua kuwa wakati huu wadhifa huo unapasa kuendea mwaniaji kutoka eneo la Afrika Mashariki.

Eneo la Kaskazini mwa Afrika nalo litatoa naibu mwenyekiti wa tume hiyo ya Umoja wa Afrika.

Aidha, mkutano huo uliofanyika Ijumaa, Machi 15, 2024 ulitupilia mbali pendekezo kwamba wadhifa huo uendee mgombeaji wa kike.

Lakini mawaziri hao waliamua kwamba ikiwa mwenyekiti wa AUC atakuwa mwanaume, naibu wake sharti awe mwanamke na ikiwa mwenyekiti atakuwa mwanamke naibu wake sharti awe mwanamume.

Kufuatia uamuzi huo, Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi alieleza kuwa “sasa ni wazi kuwa Mheshimiwa Raila Odinga atashiriki katika kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.”

“Hii ni nafasi bora kwa eneo la Afrika Mashariki kuwasilisha wagombeaji kwa nafasi ya mwenyekiti wa AUC. Kwa hivyo, hamna vikwazo vya kikanuni na kisheria vinavyoizuia Kenya kuwasilisha mgombeaji wake,” akaeleza.

Kikosi cha kuendesha kampeni za Bw Odinga kinashirikisha aliyekuwa balozi wa Kenya nchini Amerika Elkanah Odembo, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Shirika la Maendeleo Ukanda huu, (IGAD) Mahboub Maalim na Profesa Makau Mutua, ambao walifichuka kuwa wanapanga mikakati ya kushinda kiti hicho.

Kikosi hicho, kinajumuisha maafisa wote wa serikali wakiongozwa na Rais William Ruto na maafisa kutoka Wizara ya Mashauri ya Kigeni wakiongozwa na Bw Mudavadi na mabalozi ya Kenya katika mataifa yote ya Afrika.

Maafisa hao wa kibalozi wataendesha mazungumzo na wakuu wa nchi za wanakohudumu ili kuimarisha nafasi ya Odinga kushinda.

“Azma yetu ni kuwaunganisha Wakenya wote katika kumpigia debe Mheshimiwa Odinga ambaye ana maono ya kuona kwamba Afrika inaungana na kuendelea huku amani ikidumu,” Bw Mudavadi akaeleza.

Jumapili, Machi 17, 2024, Bw Odembo aliambia Taifa Dijitali kwamba Bw Odinga mwenyewe amekutana na marais kadhaa wa Afrika ambao wamekubali kumuunga mkono kwa wadhifa huo, “kando na juhudi zinazoendeshwa na Rais Ruto na Bw Mudavadi.”

Taifa Dijitali ilibaini kuwa Bw Odinga anategemea pakubwa usaidizi kutoka kwa Rais Ruto pamoja na juhudi zake mwenyewe baada ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa Rais wa Uganda Yoweri Museveni na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame.

“Bw Odinga pia amewafikia kama vile Filipe Nyusi (Msumbiji), Nana Akufo-Addo (Ghana), Felix Tshisekedi (DRC), Nangolo Mbumba (Namibia) na Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe),” Bw Odembo akaambia Taifa Dijitali.

  • Tags

You can share this post!

Kidosho anayetamba kwa kuigiza kwa lugha ya mama

Wa Muchomba aongoza kupinga ujenzi wa nyumba za bei nafuu...

T L