Mbinu mpya kupima Covid-19 kwa sekunde 30
Na BENSON MATHEKA
KENYA inapopambana na mrundiko wa sampuli unaochelewesha matokeo ya vipimo vya Covid-19 kwa zaidi ya wiki moja, hospitali moja nchini Israeli imevumbua mbinu ya kupima na kutoa matokeo katika muda wa sekunde 30.
Uvumbuzi huu wa kwanza ulimwenguni unahusisha kupima mate ya mtu, na ni moja kati ya mbinu tano ambazo wanasayansi wa Israeli wamevumbua kurahisisha upimaji wa virusi vya corona, na hivyo kuzuia visisambae kwa haraka miongoni mwa raia wake.
Israeli pia imebuni mbinu nyingine ya kutumia kifaa sawa na vuta pumzi kinachotumiwa kupima kiwango cha pombe mwilini kupima corona.
Hii ni tofauti na hapa nchini ambapo sampuli zinachukuliwa na kupimwa kwa kutegemea vifaa kutoka nje ya nchi.
Wizara ya Afya imekuwa ikikiri kwamba matokeo yamekuwa yakichelewa kwa kukosa kemikali zinazohitajika kutumiwa kupima virusi vya corona, hali ambayo imekuwa ikisababisha matokeo kuchukua zaidi ya wiki moja kutolewa.
Eli Schwartz, mtafiti katika hospitali ya Sheba Medical Center nchini Israel alisema mbinu wanayotumia ni rahisi.
Kucheleweshwa kwa matokeo nchini kumefanya walio na virusi kuendelea kuvisambaza kabla ya kubainika wameambukizwa, hasa ikizingatiwa wengi wa waathiriwa hawana dalili za virusi hivyo.
Madaktari wameelezea hofu yao kwamba huenda kiwango cha maambukizi nchini ni cha juu sana kuliko serikali inavyokadiria kutokana na idadi ndogo ya upimaji.
Dkt Robert Etali wa hospitali ya Meridian anasema mrundiko wa sampuli umevuruga vita dhidi ya janga la corona nchini.
“Mbinu inayotumiwa inajikokota sana kwa sababu inategemea vifaa na kemikali kutoka nje ya nchi ambazo ni ghali na hazipatikani kwa urahisi. Uvumbuzi kama wa Israeli unaweza kufanywa Kenya kwa sababu kuna taasisi zinazofanya utafiti wa matibabu,” asema Dkt Etali.
Kulingana na Dkt Elizebeth Gitau, Afisa Mkuu Mtendaji wa Chama cha Matabibu nchini (KMA), sampuli hazifai kuchukua zaidi ya saa 24: “Ubora wa matokeo hutegemea muda unaotumiwa kuzipima.”
Madaktari katika Kaunti ya Kiambu inayotegemea Kemri kupima sampuli zake, wamekuwa wakilalamika kuwa wanapata matokeo baada ya wiki mbili.
Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui naye amelalamika kuwa inachukua zaidi ya siku 10 kupata matokeo ya sampuli.