Habari Mseto

Mbunge adai vijana wa kiume Kisauni wanasaidiwa lakini hawaoni

June 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Kisauni Ali Mbogo amewalaumu vijana, hasa wa kiume, katika Kaunti ya Mombasa kwa kususia miradi ya maendeleo wanayoanzishiwa ili kujikimu kimaisha.

Bw Mbogo amesema imekuwa ni changamoto kubwa sana kuanzisha miradi kwa vijana wa kiume kwa sababu ya ubishi na mafarakano baina yao.

Kutokana na hulka hiyo, Bw Mbogo alisema amekwua akiegemea upande wa kina mama ambao wana umoja na wanaendeleza miradi yao bila migogoro.

“Shida kubwa watu wetu hususan vijana wetu wa jinsia ya kiume, wamekwua wakituvunja moyo. Unawaanzishia miradi muda si muda wanaanza kukosana mwishowe wanagawanya pesa na kila mtu anaenda njia zake. Hii ni changamoto kubwa sana, nimelaumiwa sana ati napendelea kina mama lakini hiyo ndio sababu kuu,” alisema Bw Mbogo akihutubu jana Jumatatu.

Alitoa mfano wa mradi wa kuosha magari aliowaanzishia vijana eneo la Mtopanga lakini ulisambaratika baada ya siku mbili.

“Waliuza vifaa wakagawanya pesa na kila mtu akaenda njia yake. Tumetimiza ahadi yetu lakini pia nyinyi mjibidiishe kama vijana. Mnaogopa fedha za vijana sababu wengi wenu mna mikopo kutoka ama Fuliza, Mshwari au Branch. Mnafaa muwe na bidii na nidhamu,” alisisitiza Bw Mbogo.

Mbunge huyo kwa upande mwingine aliwasifu kina mama akisema wanapoanzishiwa miradi huwa wanajikakamua kuhakikisha wananufaika pakubwa na maendeleo hayo.

Bw Mbogo alisema yuko tayari kusimama na vijana ili waendeleze biashara zao.

Hata hivyo, aliwataka wawe waaminifu na wenye bidii.

Alisema ataendelea kufanya uchunguzi kabla asaidie vijana ili kuhakikisha hawafuji mali na badala yake wananufaika kutokana na miradi.