Mbunge ahisi ingekuwa bora wazazi wapewe muda wa wiki mbili kujiandaa kurudisha watoto shuleni
Na LAWRENCE ONGARO
HATA ingawa serikali imeagiza shule zifunguliwe kuanzia Jumatatu wiki ijayo, baadhi ya wadau wanahisi bado kuna mambo machache yanayostahili kuwekwa sawa.
Mbunge wa Thika Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema wazazi wanastahili kupewa muda wa wiki mbili hivi ili nao waweze kujiandaa vyema kifedha.
Alisema kwa wakati huu wazazi wengi wamebanwa na hali ngumu ya maisha na kwa hivyo ni vyema kupewa muda wajipange.
“Tangazo la Waziri wa Elimu Prof George Magoha, limekuja ghafla ambapo asilimia kubwa ya wazazi hawana fedha za kuwaregesha wana wao shuleni,” alisema mbunge huyo.
Aliyasema hayo mnamo Jumatano katika afisi yake ya NG-CDF mjini Thika.
Alisema shule nyingi za msingi hazijatayarisha mazingira ya shule zao na kwa hivyo wangepewa muda wa kuweka maeneo hayo kuwa sawa.
“Walimu wakuu wa shule wanacho kibarua kikubwa mbele yao kuona ya kwamba kila kitu kinawekwa sawa ambapo bila hivyo, kutakuwa na shida wanafunzi wakirudi shuleni,” alisema Bw Wainaina.
Alisema changamoto kubwa inavyostahili kujadiliwa ni kuwa na maji kwenye matangi, vyoo ni sharti ziongezwe,na shule hizo ni lazima zifyekwe.
Alisema mipango hiyo yote katika shule nyingi hazijatimizwa na kwa hivyo bado kutakuwa na shida.
Alisema walimu watalazimika kufuata mwongozo mpya ili kuzuia au kupunguza kabisa visa vya maambukizi ya Covid-19.
“Walimu watalazimika kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanafunzi kudumisha usafi kila mara. Hata mabweni, na hata madarasa yatakuwa na wanafunzi wachache kwa mujibu wa mwongozo wa Wizara ya Afya,” alisema Bw Wainaina.
Alisema kati ya shule za msingi 56 mjini Thika, tayari 32 zimefanyiwa ukarabati huku zikiwa na maji safi ya matangi na vyoo vipya vikiwa vimejengwa.
“Tayari fedha za NG-CDF zimetumika kurekebisha shule hizo. Ninapongeza walimu wakuu wa shule hizo kwa kuonyesha ushirikiano na wajenzi wanaoendesha ukarabati huo,” alisema mbunge huyo.
Alipendekeza kwa Wizara ya Elimu kuwakubalia wanafunzi kuingia darasani hata wakiwa hawana karo ili kuwapa wazazi nafasi ya kujipanga wakitafuta.
Alisema hata wanafunzi wenyewe wana hamu kubwa ya kurejea madarasani baada ya kuwa likizoni kwa miezi saba.
“Hasa wanafunzi wa Darasa la Nane na Kidato cha Nne wanaotarajia kufanya mitihani yao wana hamu ya kukamilisha mzigo huo ulioko mbele yao. Kwa hivyo, hatua ya wao kurejea shuleni wakati huu ni muhimu sana,” alisema Bw Wainaina.