• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Mbunge akiri walimu wa shule za wamiliki binafsi wanapitia hali ngumu

Mbunge akiri walimu wa shule za wamiliki binafsi wanapitia hali ngumu

Na LAWRENCE ONGARO

WALIMU hasa wa shule za wamiliki binafsi wanapitia masaibu mengi hasa wakati huu Wakenya wanakabiliana na Covid-19.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘ Jungle’ Wainaina, anasema kwa miezi mnne sasa walimu wengi wamegeuka waombaji ambao hawana mbele wala nyuma.

“Wakati huu ukipatana na walimu hao utashuhudia msongo wa mawazo nyusoni mwao; jambo ambalo linasikitisha sana,” amesema Bw Wainaina.

Ametoa mwito kwa serikali kuu na zile za kaunti kujitokeza na kuona jinsi walimu hawa wanavyoweza kupigwa jeki ili wapate kitu cha kuweka tumboni.

“Kwa wakati huu familia nyingi kwa jumla zimegeuka kuwa ombaomba huku maisha yakizidi kuwa magumu,” amesema Bw Wainaina.

Amesema homa ya corona imegeuza karibu kila mtu kuonekana maskini kwani wengi walipoteza ajira huku wakisalia kubaki nyumbani wasijue la kufanya.

Amesema ni jambo la kusikitisha kuona ya kwamba watu wengi hawajaona mshahara ukiingia katika akaunti zao kwa miezi minne mfululizo.

Ameyasema hayo mjini Thika alipokuwa akiwahutubia waandishi wa habari.

Amesema huku walimu wakiendelea kupitia masaibu hayo, bado washika dau wanaendelea kujikuna vichwa wakishindwa kueleza hasa ni lini shule zitafunguliwa rasmi.

Kulingana na Waziri wa Elimu shughuli za masomo zitarejelewa rasmi pengine mwezi Januari 2021.

Dkt Moses Ndung’u wa mjini Thika amesema ni jambo la kusikitisha kwa sababu wanafunzi wengi hasa wasichana wadogo wamepachikwa mimba kipindi hiki kigumu cha janga la corona.

“Wanafunzi wamekosa kazi za kufanya hadi wanaonekana mitaani wakizurura ovyo bila kujali,” amesema Dkt Ndung’u.

Amesema wazazi wengi wamesongwa na mawazo mengi huku wakipatwa na msongo wa mawazo.

Amesema watu wengi kwa wakati huu wanastahili kufanyiwa ushauri wa kiakili kutokana na masaibu wanayopitia kila mara.

  • Tags

You can share this post!

Kituo cha Covid-19 kimeundwa Pumwani – Amoth

Bei ya mafuta yapanda tena

adminleo