Mbunge anyakwa na EACC kuhusu ufisadi
Na BERNARDINE MUTANU
Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Mwangi Gakuya alikamatwa Jumatano na makachero wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).
Mbunge huyo alikamatwa kuhusiana na tuhuma za kuhusika katika ufisadi, kwa kukiuka sheria za uagizaji wa bidhaa.
Alisemekana kulenga kupatia biashara ya thamani ya Sh40 milioni kampuni zake katika matumizi ya pesa za maeneo bunge (CDF).
Makachero hao walimkamata mbunge huyo katikati mwa jiji baada ya kupata idhini ya kumkamata na kumfungulia mashtaka.
Kisa hicho kiligunduliwa na benki, alimo na akaunti, baada ya kuibuka kuwa mbunge huyo alikuwa akihamisha pesa kutoka kwa akaunti ya CDF hadi akaunti zake za biashara za familia.
Msemaji wa EACC Yassin Alia alisema uchunguzi ulionyesha kuwa mbunge huyo alitumia kampuni za familia kufanya biashara.
“Kampuni hizo ilikuwa ni pamoja na zile za ujenzi katika eneo bunge hilo. Alitumia kampuni hizo kununua na kutoa bidhaa zilizofadhiliwa na CDF, kinyume na sheria,” alisema Bw Aila.
Gakuya alihojiwa wiki mbili zilizopita na wachunguzi ambapo alisema alikuwa akiwasaidia vijana ambao hawakuwa na uwezo kupata biashara ili walipwe.