Mbunge sasa ataka usaidizi zaidi kwa waliohama makazi
MBUNGE wa Kinango, Gonzi Rai, ametoa wito wa kuwepo kwa rasilimali zaidi ili kusaidia ipasavyo jamii nzima iliyoathiriwa na ujenzi wa Bwawa la Mwache hasa kujenga upya miundomsingi muhimu.
Zaidi ya familia 4,000 zinazohamishwa ili kupisha ujenzi wa bwawa hilo la mabilioni ya pesa katika Kaunti ya Kwale zinatarajia kunufaika na mpango wa kurejesha hali ya kawaida ya maisha unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa Sh1.9 bilioni.
Hata hivyo, mbunge huyo alisema ruzuku ya Benki ya Dunia ya Sh1.9 bilioni haitatosha kutatua changamoto za barabara, maji na miundomsingi ya afya katika maeneo ambayo watu walioathiriwa wanahamia.
“Watu wangu wanahamishwa kutoka eneo la mradi na kupelekwa eneo la juu la mto kwenye kata ya Mavumbo inayopakana nalo. Kwa bahati mbaya kwao, hawatafaidika moja kwa moja na maji ya bwawa kwa sababu yameundwa kuongeza usambazaji wa maji Kaunti ya Mombasa, kwa hivyo wanapaswa kutunzwa vyema,” akasema Bw Rai.
Vilevile, aliitaka wizara husika na washauri wa mradi huo kuzingatia utoaji wa fedha taslimu kwa wafanyabiashara wadogo, sawa na thamani ya vifaa vinavyopendekezwa ili kuwapa wenyeji uhuru wa kuanzisha biashara wanazotaka.
Serikali inatumia Sh4 bilioni kuwalipa fidia wakazi wa eneo la Mwache na hadi sasa Sh1.6 bilioni zimetumika kuwalipa wakulima wadogo, huku Sh2.4 bilioni zilizosalia zikitarajiwa kulipwa kuanzia Machi mwaka ujao.Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Unyunyizaji, Ephantus Kimotho, kila familia itafuatiliwa popote inapoishi ili kuhakikisha maisha yao hayakatizwi, iwe katika biashara au kilimo.
“Mpango ambao tayari unatekelezwa utasaidia jamii kupunguza athari mbaya za kuhama na kuendeleza shughuli mbalimbali za kiriziki,” Bw Kimotho aliambia wanahabari wakati wa ziara kwenye mradi huo.
Bw Kimotho alisema kati ya ruzuku ya Benki ya Dunia ya Sh1.9 bilioni, Sh450 milioni zitatumika kupata ardhi na kujenga upya shule tatu mpya za umma.Shule hizo ni za msingi za Fulugani na Kunguni, na chekechea ya Mwache Bridge, kila moja ikiwa na vifaa vya kisasa vya masomo.
Sh390 milioni nyingine zitatumika kununua pembejeo za kilimo kwa ajili ya kusaidia familia zilizohamishwa ambazo zilikuwa zikijishughulisha na biashara ya kilimo au ufugaji, na kusaidia viwanda vidogo na vidogo.
Sh1.1 bilioni zilizobaki zitatumika kujenga miradi ya miundomsingi ya jamii ikiwemo barabara, maji na vituo vya afya.