Habari Mseto

Mbunge wa Gatundu Kaskazini abadilisha wimbo baada ya Gachagua kukohoa

January 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

MBUNGE Elijah Kururia wa Gatundu Kaskazini ameonekana kubadilisha msimamo wake wa kumuunga mkono mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu) kuwa kiongozi na msemaji wa Mlima Kenya.

Bw Kururia, aliyechaguliwa kama mwaniaji huru kwenye uchaguzi wa Agosti 9, 2022, alikuwa miongoni mwa wabunge karibu 15 waliotangaza kumuunga mkono Bw Nyoro kuwania urais 2032 mnamo Ijumaa, Januari 12, 2024.

Wabunge hao walitoa tangazo hilo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Masomo Bora katika uwanja wa michezo wa Mumbi, eneobunge la Kiharu, Kaunti ya Murang’a.

Licha ya kuwa miongoni mwa wabunge hao, Bw Kururia alionekana kubadili msimamo wake mnamo Jumapili, akisema kuwa kwa sasa Naibu Rais Rigathi Gachagua ndiye kiongozi wa kisiasa wa ukanda huo.

“Kwa sasa, kiongozi wetu ni Naibu Rais Gachagua. Tutamuunga mkono hadi mwisho. Hata hivyo, hilo halimaanishi kuwa viongozi wengine hawafai kujipanga kisiasa,” akasema Bw Kururia, kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio.

Kwenye mahojiano hayo, Bw Kururia alionekana kujitenga na ubabe wa kisiasa ambao umekuwa ukiandelea baina ya Bw Gachagua na Bw Nyoro, badala yake akisema kuwa lazima eneo hilo lizungumze kwa sauti moja ili “kutimiza malengo yake ya kisiasa”.

“Lazima tuvumiliane kama wenyeji wa Mlima Kenya. Lazima viongozi waliopo wawe kielelezo chema kwa vijana. Si vizuri tukipanda mbegu ya mizozo na mivutano isiyoisha baina yetu,” akaeleza mbunge huyo.

Mbunge huyo alisema kuwa yuko huru kuunga mrengo wowote, kwani hana kikwazo chochote cha kisiasa.

Hata hivyo, mbunge huyo alilalamikia kutofaulu kwa Mpango wa Maridhiano (BBI), akisema kuwa ndiyo njia ya kipekee amayo ingelifaa eneo hilo, kwani ulijumuisha mfumo wa Kura Moja-Shilingi Moja-Mtu Mmoja, uliolenga kulisaidia kuongeza mgao wake wa fedha.

Mpango huo ulianzishwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, kupitia handisheki baina yao mnamo 2018.