Mbunge wa Thika asisitiza sharti serikali iendelee kukabiliana na mafisadi
Na LAWRENCE ONGARO
SERIKALI imehimizwa kukabiliana na mafisadi kwa nguvu zote zilizoko.
Mbunge wa Thika Mhandisi Patrick ‘ ‘Jungle’ Wainaina, alisema Ijumaa msimamo wa serikali kuhusu ufisadi haustahili kulegezwa hata kidogo.
“Tunaunga mkono taarifa ya juzi ya Rais Uhuru Kenyatta aliyotoa bungeni kwa kusisitiza ya kwamba yeyote katika afisi kubwa akitajwa tu na asasi faafu kisheria kuhusu maswala ya ufisadi, anastahili kujiondoa afisini ili uchunguzi ufanywe dhidi yake,” alisema Bw Wainaina.
Alitoa mwito kwa taasisi husika za kukabiliana na ufisadi ziendeshe kazi yao kimya ili wahusika wasiendeleze siasa kuzihusu.
“Uchunguzi wa ufisadi usifanywe kupitia vyombo vya habari, bali uwasilishwe mahakamani baada ya ushahidi kamili kupatikana,” alisema Bw Wainaina.
Alisema kwa sababu ufisadi umekithiri zaidi, watafanya juhudi kupitisha mswada wa kutaka mafisadi wakinaswa wakatwe mikono na miguu ili uwe ujumbe mkali kwao.
Aliyasema hayo mnamo Ijumaa alipozuru shule za upili za Karibaribi Girls Secondary na Karibaribi Mixed Secondary, kufungua miradi ya maendeleo.
Alisema shule ya Karibaribi Girls ilipata bweni, nayo ya Karibaribi Mixed Secondary, ilipata maabara, darasa, na choo cha shule.
Alisema katika bajeti ya 2018-19, atatumia takribani Sh58 milioni kukarabati shule 50 zilizoko eneo lake la uwakilishi la Thika.
Alitoa mwito kwa vijana kujiamini na kuanzisha biashara ili waweze kujiendeleza kimaisha.
“Ninawapa ujumbe kuwa siku hizi kazi za ofisi zimekuwa adimu kupata. Kwa hivyo, ni vyema kuungana kwa vikundi na kuanzisha miradi tofauti ili kujikimu kimaisha,” alisema Bw Wainaina.
Mikopo
Alisema watafanya juhudi kuona ya kwamba ajenda nne za serikali zinazingatiwa na wakazi wa Thika, mradi tu wapewe mikopo kupitia serikali.
Aliitaka serikali kuwapiga jeki walio katika vikundi vinavyotaka kuendesha biashara.
“Kandarasi ya kujenga nyumba za kuishi inastahili kupewa Wakenya ili nao wapate njia ya kuendeleza maisha yao,” alisema Bw Wainaina.
Alisema anapinga Wachina kupewa kandarasi ya ujenzi wa nyumba katika Kaunti zetu.
“Nafasi hiyo ipewe watu wetu wa hapa nchini ili wafaidike kimaisha,” alisema Bw Wainaina.
Alisema kwa muda wa miaka mitatu ijayo watafanya juhudi kuona ya kwamba shule zote za msingi na upili zinapata sura mpya ili kuwapa wanafunzi motisha kusoma vyema.
Alitoa mwito kwa wahisani pia wajitokeze kusaidia katika miradi tofauti ili kufanikisha maendeleo ya Thika kwa ujumla.