Mbunge wa zamani asimulia alivyostawisha mtaa wa kifahari
Na RICHARD MUNGUTI
ALIYEKUWA Mbunge wa Tetu James Ndung’u Gethenji Jumatatu alieleza mahakama kuu kwamba alistawisha mtaa wa kifahari wa Kihingo ulioko eneo la Kitsuru jijini Nairobi kwa bei ya zaidi ya Sh800 milioni.
Bw Gethenji alimweleza Jaji David Majanja kwamba alitumia muda wa miaka isiyozidi mitatu kustawisha nyumba 55 za kifahari zenye thamani ya Sh20 bilioni alizowauzia wawekezaji wa humu nchini na kimataifa.
Akiongozwa kutoa ushahidi na wakili Willis Otieno mbunge huyo wa zamani wa Tetu alisema ndiye mwenyekiti wa kampuni ya Kihingo Village (Waridi) Gardens Limited (KVWGL) iliyopewa mkopo wa kuzistawisha.
Kwa mujibu wa sheria zinazothibiti kampuni hiyo wawekezaji walionunua nyumba hizo walikubaliwa kushiriki katika mikutano ya kampuni hiyo baada ya kupewa hisa moja kila mmoja.
Hata hivyo alisema mzozo uliibuka kati yake na ndugu yake mkubwa Gitahi Gethenji kuhusu usimamizi na umiliki wa hisa za kampuni hiyo.
Akitoa ushahidi mbele ya Jaji David Majanja, Bw Gethenji alibaini kwamba usimamizi wa majumba 55 ya kifahari upo chini ya KVWGL.
Alisema kampuni hiyo iko na hisa 115 na kwamba kampuni iliyoistawisha imepewa hisa 60.
Wakati wa mikutano ya upigaji kura kampuni ya Kihingo imepewa mamlaka makubwa kwa vile iko na hisa 60.
“Sheria za kampuni zimenipa mamlaka na uwezo wa kusimamia shughuli za kila siku za Kihingo,” alisema Bw Gethenji.
Wakati wa mikutano ya kujadili masuala ya mtaa wao, mmoja wa wamiliki wa nyumba hapo William Pike alizua masuala kadhaa.
Bw Gethenji na pia mkurugenzi mwingine Julius Chacha Mabanga walisema mtafaruku ulizuka wakati wa mkutano wa kampuni hiyo hata ikamlazimu mbunge huyo wa zamani kushindwa kuthibiti mkutano huo.
Wakihojiwa na wakili Allen Gichuhi Mabw Gethenji na Mabanga walisema kwamba kampuni ya Kihingo ndiyo iliyo na mamlaka ya kusimamia mtaa huo wa kifahari.
Bw Gichuhi alimhoji jinsi Bw Mabanga aliteuliwa. “Nilikabidhiwa barua nikiteuliwa kuwa mkurugenzi wa Kihingo,” alisema Bw Mabanga.
Mkurugenzi huyo alisema ijapokuwa msajili wa makampuni aliharamisha kuteuliwa kwake angali mkurugenzi baada ya mtafaruku uliokuwa kusuluhishwa.
Kesi inaendelea.