Habari Mseto

MCA watupwa nje ya basi kwa kudai marupurupu njiani

June 6th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WANYORO

MADIWANI watano wa Kaunti ya Embu walishtuka walipofurushwa kutoka kwa basi na kuachwa barabarani baada ya kutofautiana na Afisa Mkuu na waziri mmoja wa kaunti hiyo kuhusu marupurupu wakati wa safari yao kuelekea Mombasa.

Madiwani hao walikuwa wamealikwa na waziri huyo, kwenye ziara maalum ya mafunzo jijii Mombasa.

Madiwani, ambao walijumuisha diwani maalum mlemavu na mhubiri wa kanisa la Kianglikana (ACK) walilazimika kushuka katika basi ambalo walikuwa wakisafiria karibu na mji wa Machakos.

Madiwani hao wote ni wanachama wa Kamati ya Jinsia, Utamaduni na Huduma za Watoto na walikuwa wamealikwa kwa ziara ya kujifunza kuhusu biashara ya ushonaji mjini humo.

Viongozi hao walijumuisha Sicily Warue (mwenyekiti), madiwani Newton Kariuki, Patrick Mukavi, Mhubiri Elizabeth Kibai na Bw Bernard Kandia, ambaye anawakilisha walemavu. Waliachwa huku wenzao wakielekea jijini Mombasa.

Viongozi hao walirudi mjini Embu kwa kutumia magari ya usafiri wa umma.

Aidha, walikuwa wamealikwa na Waziri wa Jinsia Joan Mwende, lakini Mkuu wa Uajiri Jane Ndegi akakataa kukubali maombi yao. Aliamuru waachwe na basi ambalo lilikuwa likiwasafirisha.

Picha zilizosambazwa mtandaoni zilionyesha viongozi hao wakiwa wametamauka. Bw Kibai alisema kuwa picha hiyo ilipigwa na waziri huyo.

Madiwani wengine maalum walielekea Mombasa bila ya kufahamu ikiwa ziara hiyo ingefanikiwa au la.

Akizungumza mjini Embu, Bi Warue alisema kwamba kumekuwa na malumbano katika wizara hiyo kuhusu udhibiti wa Sh15m ambazo zimetengewa uimarishaji wa sekta ya ushonaji.

Alisema kuna mzozo wa kimamlaka kati ya Dkt Mwende na Bi Mugambi. Alimlaumu mkuu huyo kwa kupuuzilia mbali maamuzi ya mkubwa wake.

Bi Warue alisema kwamba kamati hiyo itafufua mipango ya ziara hiyo upya wakati tofauti za maafisa hao wawili zitasuluhishwa. Madiwani hao waliwatahadharisha maafisa hao dhidi ya kuwaingiza katika mzozo wao.

Diwani mmoja ambaye hakutaka kutajwa alisema walichukua hatua hiyo ili kuepuka “kusumbuliwa” wakiwa Mombasa. Katibu wa Bunge la Kaunti Jim Kauma alithibitisha tukio hilo.