• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 AM
MCAs waliovujisha video ya spika ‘akilazimisha’ mwanamke amkumbatie kuitwa kujitetea

MCAs waliovujisha video ya spika ‘akilazimisha’ mwanamke amkumbatie kuitwa kujitetea

NA WINNIE ONYANDO

MADIWANI wawili wa Kaunti ya Nairobi watalazimika kufika mbele ya Kamati ya Mamlaka ya Hadhi ya Bunge kueleza ni kwa nini walisambaza video iliyoonyesha Spika wa kaunti hiyo Kennedy Ng’ondi akimlazimisha diwani wa dini ya Kiislamu kumkumbatia.

Akiwahutubia wanahabari, Diwani wa Makongeni Peter Imwatok aliwakemea madiwani hao akisema kwamba video hiyo inalenga kumharibia jina spika Ng’ondi.

“Tayari nimepewa majina ya madiwani hao wawili na nitayawasilisha mbele ya kamati ya Mamlaka ya Hadhi ya Bunge kujitetea,”

“Suala hilo limechukuliwa kwa uzito na kuwasilishwa mbele ya Kamati hiyo na wahusika watachukuliwa hatua,” akasema Bw Imwatok.

Kwa upande wake, Spika Ng’ondi alijitetea akisema kwamba video hiyo ilichukuliwa 2022 wakisherehekea siku yake ya kuzaliwa.

“Video hiyo ilichukuliwa 2022. Sherehe hiyo iliandaliwa na madiwani wanawake. Sikuwa na nia mbaya. Kadhalika, ninawaheshimu sana akina dada na hasa wale wa dini la Kiislamu,” akasema Bw Ng’ondi.

Kando na hayo, spika huyo alimpigia simu diwani huyo huku akieleza kuwa anamheshimu kama kiongozi mwenzake.

Kwenye video hiyo, Bw Ng’ondi alionekana akimlazimisha diwani huyo wa kike kusimama na kumkumbatia mbele ya viongozi wenzake.

Video hiyo ilivutia makini ya watu hasa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii huku wengi wakimshambulia spika huyo kwa kitendo hicho walichokiita unyanyasaji wa kimapenzi.

  • Tags

You can share this post!

Instagram ilinipa mume, asema Rev Lucy Natasha

Polisi sasa wagundua mbinu mpya zinazotumiwa na wauzaji...

T L