Mchuuzi kushtakiwa kwa mauaji ya mhudumu wa choo
MCHUUZI anayeshukiwa kutekeleza mauaji ya mhudumu wa choo cha umma kwenye soko la wazi la Muthurwa, Kaunti ya Nairobi atazuiliwa kwa muda wa siku 14 ili uchunguzi kufanyika.
Collins Oduor Wangira almaarufu Vampire (mnywa damu ya binadamu) aliyeagizwa asalie katika kituo cha polisi cha Kamkunji hadi Julai 29,2024 ili kuhojiwa zaidi, atashtakiwa kwa mauaji ya Boniface Opiyo mnamo Julai 10, 2024.
“Opiyo alidungwa visu na kundi la vijana saba waliomvamia katika choo cha umma anakofanya kazi na kumjeruhi vibaya,” afisa wa polisi, Konstebo Pwoka Mauka alimweleza Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Milimani, Bi Dolphina Alego.
Kufuatia uvamizi huo ulioongozwa na Wangira, Opiyo alipata majeraha mabaya kisha akakimbizwa katika Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) na nduguye.
“Mshukiwa katika kesi hii alikamatwa Julai 11, 2024 kufuatia madai ya kumshambulia Opiyo katika soko la wazi la Muthurwa,” Konstebo Mauka alimweleza Bi Alego.
Afisa anayechunguza kesi hiyo alieleza mahakama kwamba anahitaji siku 14 kukamilisha uchunguzi.
“Wangira alikuwa ameandamana na marafiki zake walipomshambulia Opiyo kwa kumdunga na visu na kumjeruhi vibaya. Walimzingira katika choo cha umma anakofanyakazi na kumshambulia,” Konstebo Mauka alieleza korti.
Hakimu alielezwa kuwa Wangira atafunguliwa mashtaka ya mauaji kinyume cha sheria nambari 203/204 cha sheria za jinai.
Mahakama ilifahamishwa kuwa Opiyo alikata roho alipokuwa anaendelea kupokea matibabu KNH.
“Mshtakiwa alikuwa anaendelea na kazi zake Fresh Life Toilet (choo cha umma) alipovamiwa na watu saba wakiongozwa na Wangira. Walimshambulia na kumwumiza,” alisema Konstebo Mauka.
Hakimu alielezwa washukiwa waliwatupia mawe na vipande vya chupa vilivyovunjika watu waliosongea kumwokoa Opiyo.
Opiyo aliponyoka kutoka kwa washambulizi wake kisha akakimbilia usalama wake katika kituo kidogo cha polisi cha Muthurwa, lakini Wangira na wenzake wakamshinda mbio, wakamkamata na kumshambulia zaidi kisha wakatawanyika.
Mahakama ilifahamishwa Wangira aliuguza majeraha pajani aliposhambuliwa na wananchi alipojaribu kutoroka.
Alikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha Polisi cha Kamkunji kuhojiwa.
Uchunguzi zaidi umedhihirisha kuwa Wangira hajapokea kitambulisho cha kitaifa licha ya kutimiza umri wa kupata cheti hiki muhimu.
Konstebo Mauka aliomba korti iruhusu ombi lake la kumzuilia Wangira kwa siku 14, ili akamilishe uchunguzi na kuandikisha taarifa za mashahidi sawia na kumpeleka kupimwa wazimu katika Hospitali ya Mathari.
“Baada ya kutathmini ushahidi wote, nimefikia uamuzi kwamba polisi wanahitaji muda wa kukamilisha uchunguzi,” alisema Bi Alego.
Mahakama iliamuru azuiliwe kwa siku 14 kukamilisha uchunguzi.
Kesi itatajwa Julai 29, 2024 kwa maagizo zaidi.