MCK kortini kudai fidia ya wanahabari waliojeruhiwa na mabaunsa
NA FRIDAH OKACHI
BARAZA la wanahabari Nchini (MCK), limewasilisha kesi dhidi ya mmiliki na wafanyakazi wa usalama wa Kettle House Bar and Grill jijini Nairobi, kudai fidia ya wanahabari waliojeruhiwa, wakati wa msako uliofanywa na Mamlaka ya Kitaifa Dhidi ya Matumizi Mabaya ya Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA).
Akizungumza mjini Nyandarua, Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza hilo, Bw David Omwoyo, alisema MCK itashinikiza fidia kwa wanahabari waliopata majeraha ya kimwili na vifaa vyao kuharibiwa Januari 6, 2024.
“Wakati huu, tumeamua kupiga hatua zaidi. Tunaenda kortini kudai fidia ya uvamizi huo,” alisema Bw Omwoyo.
“Kesi hiyo ya uhalifu ikiendelea, Baraza linaamini kuwa fidia hiyo ni njia mojawapo kukomesha vitisho na majeraha kwa wanahabari. Pia itawajibisha watu wenye mazoea ya kuhujumu kazi za vyombo vya habari na kuingilia uhuru wake,” aliongeza.
Bw Omwoyo alionya wamiliki wa biashara wanaounga mashambulio kwa wanahabari wenye vibali wakiwa kazini, akisema kuwa hatua zitachukuliwa dhidi yao.
Wakati huo huo, aliwashauri wanahabari kuwa waangalifu wakati wa kufanya kazi katika mazingira yasiyo salama.