Habari Mseto

Meneja wa benki akana kuwasaidia magaidi wa shambulizi la Riverside

February 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MENEJA wa Benki ya Diamond Trust (DTB) tawi la Eastleigh Nairobi alishtakiwa Jumatano kwa kuwasaidia magaidi kutekeleza shambulizi la hoteli ya Dusit D2 ambapo watu 21 waliuawa.

Bi Sophia Njoki Mbogo (pichani) alifunguliwa mashtaka matatu ya kufanikisha shambulizi la kigaidi la Januari 15, 2019 la hoteli la Dusit D2.

Bi Mbogo alikanusha mashtaka matatu dhidi yake na wakili Jaji (mstaafu) Nicholas Ombija akaomba aachiliwe kwa dhamana.

Kiongozi wa mashtaka Bw Eddy Kadebe alipinga ombi hilo la Bi Mbogo kuachiliwa kwa dhamana akisema “ uchunguzi wa kina unaendelea kufanywa kubaini jinsi benki hiyo ilihusika katika shughuli za kigaidi.”

Jaji Ombija alimsihi hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Bw  Francis Andayi  amwachilie mshtakiwa akisema “ amekuwa korokoroni kwa muda wa siku 30 tangu atiwe nguvuni.”

Mahakama ilifahamishwa mshtakiwa alikuwa anatekeleza majukumu yake ya kazi na hakuhusika na vitendo vya ugaidi.

Bi Mbogo alifikishwa kortini mwezi uliopita pamoja na washukiwa wengine watano na kuzuiliwa kuhojiwa kuhusiana na shambulizi hilo.

Shtaka la kwanza dhidi yake lasema kuwa kati ya Desemba 4 na Januari 5 2019 katika tawi la Eastleigh la benki ya DTB alifanikisha ugaidi kwa kuwapa washukiwa wa ugaidi huo Sh34,736,550 zinazodaiwa zilitumika kwa kufadhili washambulizi la hoteli ya DusitD2 mnamo Januari 15 mwaka huu.

Bi Mbogo alikabiliwa na shtaka la pili la kukosa kutoa habari kwa maafisa wa usalama kuhusu mamilioni ya pesa yaliyokuwa yakitolewa na mteja wa benki hiyo anayeshukiwa alikuwa anawapelekea magaidi wa Al Shabaab nchini Somalia.

Shtaka la tatu lilisema alikosa kwa kutoeleza Benki Kuu ya Kenya (CBK) kwamba mteja wa benki hiyo alikuwa anatoa pesa zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa cha Dola za Marekani ($) 10, 000 (Sh 1milioni).

Kesi inaendelea.