Habari Mseto

Meneja wa Benki ya Cooperative aliyefutwa kazi kwa kupapasa mwenzake wa kike apoteza kesi

Na JOSEPH WANGUI April 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA imedumisha kufutwa kazi kwa meneja mmoja wa benki kwa kosa la kupapasa makalio ya karani wa kike kama ishara ya kumpongeza kwa utendakazi mzuri.

Kitendo hicho, ambacho mwanamume huyo alidai hakikuwa na malengo mabaya, kilitendeka baada ya kazi ya siku katika Benki ya Co-operative wakati wa kuthibitisha hesabu za pesa.

Akijieleza kama bosi mwadilifu, mwanamume huyo alisema alimgusa mwanamke huyo kutokana na furaha kwamba karani huyo alikamilisha siku bila changamoto zozote.

Meneja huyo anayesimamia shughuli za kutuma pesa, na ambaye amehudumu katika benki hiyo kwa miaka tisa alikana madai kuwa alimdhulumu mwenzake wa kike kimapenzi.

Aidha, alikabiliwa na tuhuma za kutoa kauli zisizofaa kuhusu mfanyakazi mwingine wa kike, ambaye walipenda kuzungumza naye mara kadhaa kazini. Visa hivyo viwili vilifasiriwa kama dhuluma za kimapenzi na mienendo mibaya.

Majina ya wahusika katika kesi hiyo yalibanwa ili kulinda hadhi yao. Mwanamume huyo alishangaa kwamba benki hiyo ilimfuta kazi mnamo Mei 2016 kwa misingi ya matukio hayo mawili.

Uamuzi huo sasa umedumishwa na Mahakama ya Uajiri na Mahusiano ya Leba ambayo imetupilia mbali rufaa yake dhidi ya uamuzi wa benki hiyo.

Jaji Christine Baari alisema la muhimu ni kwamba mwathiriwa alifasiri kitendo cha meneja huyo kama kisichomfurahisha.

“Isitoshe, mwanamume huyo alikubali kuwa mienendo yake haikuwafurahisha walalamishi. Kwa hivyo, alikiuka kanuni ya benki hiyo kuhusu unyanyasaji wa kingono. Pia, mahakama ilizingatia kuwa mwanamume huyo alikuwa mkubwa wa mlalamishi kazini na hivyo angejizuia,” akasema jaji huyo katika uamuzi.

Mahakama hiyo iliongeza kuwa benki hiyo ilikuwa na sababu tosha za kumfuta kazi meneja huyo.Ilieleza kuwa hatua hiyo ilikuwa ya haki na iliyochukuliwa kisheria.

Kupitia stakabadhi alizowasilisha mahakamani, mwanamume huyo alitaka Jaji Baari kuamua kwamba hatua hiyo ya kumpiga kalamu ilikuwa haramu na isiyozingatia haki.

Alisisitiza kuwa hakulenga kuwadhulumu wanawake hao na kwamba vitendo vyake vilikuwa vya mzaha tu.

Alisema kuwa mnamo Jumamosi, Aprili 2, 2016 ilikuwa wajibu wake kama meneja wa shughuli kukagua pesa za makarani wa malipo baada ya siku kuhakikisha kuwa kiasi cha pesa mitamboni kililingana na pesa za kawaida.

Mwanamume huyo aliambia mahakama hiyo ya Masuala ya Wafanyakazi kwamba mwanamke huyo hakuonekana kuchukizwa na kitendo chake cha kumpapasa makalio.