Mfanyabiashara matatani kwa kukwepa kesi mara mbili
NA RICHARD MUNGUTI
MFANYABIASHARA aliyekwepa kufika mahakamani kujibu kesi ya ulaghai wa Sh251,000 mara mbili mnamo Desemba 2023 ameshtakiwa na kunyimwa dhamana.
Hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Gilbert Shikwe aliamuru Billy Mogire Monyancha azuiliwe katika gereza la Industrial Area kwa siku mbili kabla ya kutoa uamuzi endapo atapewa dhamana au atakaa gerezani hadi kesi isikilizwe na kuamuliwa.
Akiomba Monyancha anyimwe dhamana, kiongozi wa mashtaka alieleza hakimu kwamba mshtakiwa alikosa kufika kortini Desemba 16 na Desemba 27, 2023, kujibu shtaka.
Mahakama ilielezwa mshtakiwa hakutoa sababu za kutofika kortini, hali iliyofanya hakimu mwandamizi Bi Dolphina Alego kutoa kibali Monyancha akamatwe na kufikishwa kortini.
Mahakama ilifahamishwa kwamba polisi walimsaka na jitihada zao zilifanikiwa Januari 5, 2024, walipomtia nguvuni mshukiwa huyu wa ulaghai.
Bw Shikwe alielezwa na kiongozi wa mashtaka kwamba mshtakiwa hastahili kuachiliwa kwa dhamana kwa “vile amedhihirisha haheshimu korti kwa vile amekwepa kufika kortini maradufu.”
Hakimu aliombwa aamuru mshtakiwa azuiliwe gerezani hadi kesi inayomkabili isikizwe na kuamuliwa.
Lakini mshtakiwa aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana akisema “ni haki yangu.”
Alisema upande wa mashtaka haujawasilisha ushahidi wowote kuthibitisha kwamba “hatafika kortini siku ya kusikilizwa kwa kesi.”
Hata hivyo, upande wa mashtaka ulisema mshtakiwa alihepa kufika kortini.
“Mshtakiwa haaminiki. Akiachiliwa kwa dhamana atatoroka,” kiongozi wa mashtaka alimweleza hakimu.
Akitoa uamuzi, hakimu alisema mshtakiwa atasalia gerezani kwa siku tatu.
Mshtakiwa anakabiliwa na shtaka la kuilaghai kampuni ya kuuza kompyuta ya Jossnad Sh251,000 akijifanya alikuwa na uwezo wa kuiuzia tarakilishi 14 na vipuri mbalimbali vya kielektroniki.
Mahakama ilielezwa mshtakiwa alinyakua pesa hizo mnamo Machi 31, 2023.
Mshtakiwa alikana shtaka linalomkabili.