• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Mfugaji mamba apata hasara kuu

Mfugaji mamba apata hasara kuu

Na CHARLES LWANGA

Shamba la mamba mjini Malindi limefuta wafanyakazi 10 kutokana na hali ngumu ya uchumi iliyosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona ulimwenguni.

Bi Mildred Parker, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa shamba hilo linalojulikana kama ‘Kazuri London Crocodile Farm’ kijijini Kakokeni, alisema alipunguza idadi ya wafanyakazi mwezi Aprili baada ya kupata hasara ya mamilioni ya pesa.

“Hii ni baada ya viwanda nchini Italia ambapo mimi hupeleka ngozi za mamba kuunda mikoba na mavazi mengine ya urembo kufungwa kutokana na mlipuko wa corona,” alisema.

Kulingana na Bi Parker, ambaye ni raia wa Uingereza, shamba hilo lilimgharimu takriban Sh150 milioni, na alilianzisha 2012.

Bi Parker amefuga mamba wapatao elfu moja kwa ajili ya ngozi zao ambazo huzisafirisha nchini Italia kuunda mikoba, mishipi na mavazi ya aina tofauti tofauti na nchini Uingereza ambapo mkoba mmoja huuzwa kwa hadi Sh5 milioni.

“Baada ya kuwachinja mamba na kuwabandua ngozi, mimi huchukua miaka mitatu kutengeneza mikoba hiyo, hii inatokana na uwepo wa wafanyabiashara wengi viwandani ambao pia wanasubiri huduma hiyo,” alisema.

Baadhi ya wafanyakazi ambao walifutwa kazi, alisema, ni wale ambao wamekuwa wakifanya kazi ofisini nchini Kenya na Uingereza kama vile karani, kupokea na kujibu jumbe na kubakisha wachache ambao wanafanya kazi ya kusafisha, kulinda na kulisha mamba hao katika kijiji cha Kakoneni.

Alisema kuwa biashara yake iliathiriwa na kusitishwa kwa safari za ndege na marufuku ya kuingia na kutoka kaunti ya Kilifi, Mombasa na Kwale.

“Ufugaji mamba haukuidhinishwa katika baadhi ya huduma muhimu ili kutuwezesha kuokoa biashara,” alisema.

Hata hivyo, Bi Parker alielezea matumaini ya kurejea katika biashara ingawaje huenda ikamchukua hata mwaka kabla ya kurejelea hali nzuri ya kiuchumi kama ilivyokuwa kabla ya janga la corona.

“Hii ni kwa sababu baadhi ya nchi kadhaa zimeanza kufungua biashara na nina matumaini Kenya itafungua hivi karibuni,” alisema.

Ingawaje, aliomba serikali ipunguze ushuru wa kusafirisha ngozi ya mamba nga’mbo ili kuimarisha sekta ya ufugaji wa mamba nchini.

“Ili kufanya biashara hii, lazima uwe na kibali kutoka Shirika la Huduma za Wanyama pori (KWS), mamba hao hutolewa Mto Tana, ambapo mimi huajiri wakazi kutafuta mayai ya mamba ili kuyaangua,” aliongeza.

You can share this post!

Wakenya wanataka makanisa yafunguliwe – Ripoti

Washukiwa waliokamatwa na nyama ya twiga Garissa...

adminleo